ZANZIBAR KUNADI UTALII, UTAMADUNI NA URITHI WAKE KATIKA MAONYESHO YA KILI FAIR
Na Woinde Shizza, Arusha
Zanzibar imeendelea kutumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Kili Fair kama jukwaa la kutangaza bidhaa zake za utalii, utamaduni na urithi wa kihistoria, huku ikiwakaribisha wageni na wadau wa sekta hiyo kushiriki siku maalumu ya Zanzibar itakayofanyika Jumapili.
Akizungumza katika maonesho hayo yanayoendelea jijini Arusha, Meneja wa Uhusiano wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hakimu Kimara, alisema siku hiyo maalumu itatoa fursa kwa washiriki kujifunza na kushuhudia mambo mbalimbali yanayoifanya Zanzibar kuwa moja ya vivutio vikubwa vya utalii nchini na duniani.
Alisema Zanzibar ni visiwa vilivyobeba historia ya mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa karne nyingi, jambo ambalo limechangia kujengwa kwa utamaduni wa kipekee unaoakisi mchanganyiko wa tamaduni za Kiafrika, Kiarabu na Kibantu.
Kimara alisema wageni watakaotembelea banda la Zanzibar watapata nafasi ya kujifunza kuhusu tamaduni za Wazanzibari, historia ya visiwa hivyo pamoja na urithi wake mkubwa wa kihistoria unaoifanya Zanzibar kutambulika kama moja ya maeneo tajiri katika mambo ya kale na utamaduni wa Afrika Mashariki.
Aidha, alisema washiriki watajionea vyakula vya asili vya Kizanzibari vinavyojulikana kwa ladha na mapishi yake ya kipekee yaliyoathiriwa na tamaduni mbalimbali zilizokutana katika visiwa hivyo kwa miaka mingi.
“Ukitembelea Zanzibar utakutana na vyakula vyenye mchanganyiko wa tamaduni za Kiarabu na Kibantu, jambo ambalo limeifanya Zanzibar kuwa na utambulisho wake wa kipekee katika sekta ya utalii wa utamaduni,” alisema.
Pia alisema kutakuwa na maonesho ya muziki wa asili ikiwemo taarab, ambapo wageni watapata fursa ya kufahamu historia ya muziki huo, namna ulivyobadilika kulingana na nyakati na sababu zilizochangia mageuzi hayo huku ukiendelea kuhifadhi utambulisho wake wa asili.
Kwa mujibu wa Kimara, sekta ya utalii imeendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi kwa kuingiza mapato makubwa na kuchochea ukuaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Alisema utalii ni sekta mtambuka inayogusa maeneo mengi ya uchumi kwa wakati mmoja, ikiwemo biashara, usafirishaji, malazi, huduma za chakula, sanaa na shughuli za wajasiriamali, huku ikiwaunganisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
“Utalii unawakutanisha watu wa mataifa tofauti, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka pande mbalimbali za dunia ,Kupitia maonesho kama haya tunapata nafasi ya kutangaza vivutio vyetu na kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema.
Aliongeza kuwa Maonesho ya Kili Fair yamekuwa yakitoa elimu muhimu kwa wageni na wadau wa utalii kuhusu maeneo mbalimbali ya vivutio nchini, hali inayowafanya watu wengi kufahamu maeneo ambayo hawakuwahi kuyatembelea na kupanga safari za kuyatembelea siku zijazo.
Kimara alisema maonesho hayo pia yamekuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara kwa kuwawezesha wadau wa sekta ya utalii kutangaza huduma na bidhaa zao pamoja na kujenga ushirikiano wa kibiashara na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Aidha, alitoa wito kwa mikoa mingine yenye vivutio vya utalii kuandaa maonesho yanayofanana na Kili Fair ili kuongeza juhudi za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake katika masoko ya kimataifa.
Alisema kutokana na kuongezeka kwa idadi ya washiriki na wadau wanaoshiriki kila mwaka, kuna umuhimu wa kuendelea kupanua eneo la maonesho hayo ili kutoa nafasi kwa washiriki wengi zaidi.
“Matarajio yetu ni kuona mwakani watu wengi zaidi wakishiriki maonesho haya ,Kadri tunavyoongeza majukwaa ya kutangaza utalii ndivyo tunavyoongeza fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema.
Maonesho ya Kili Fair yameendelea kujidhihirisha kuwa moja ya majukwaa makubwa ya utalii nchini kwa kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku yakichangia kutangaza vivutio vya utalii, kuimarisha biashara na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika sekta hiyo.








0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia