NISHATI SAFI YAJENGA AFYA, YALINDA MAZINGIRA NA KUINUA UCHUMI WA JAMII



Na Woinde Shizza,Arusha

Jamii imetakiwa kuachana na utegemezi wa kuni na mkaa na kuhamia matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha afya za wananchi na kuongeza fursa za kiuchumi.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa kampuni ya HANNY G Investment Hanny Mbarie, alipokuwa akizungumza kuhusu mchango wa nishati safi katika maendeleo ya jamii na juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini.

Alisema matumizi ya kuni na mkaa yameendelea kuwa chanzo kikubwa cha ukataji miti, uharibifu wa mazingira na magonjwa yanayotokana na moshi wa jikoni, hali inayowaathiri zaidi wanawake na watoto.

Alieleza kuwa kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida zake kwa afya, mazingira na maendeleo ya uchumi wa familia.

Kwa mujibu wake alisema wamekuwa wakizalisha , baadhi ya bidhaa za nishati safi  kwa kutumia mabaki ya mazao ya kilimo kama maganda ya karanga na malighafi nyingine zinazopatikana kwa urahisi, hatua inayochangia kuongeza thamani ya mazao hayo na kutoa fursa za ajira.

Alisema matumizi ya nishati safi yanasaidia kupunguza muda unaotumika kutafuta kuni na hivyo kuwawezesha wananchi kushiriki zaidi katika shughuli za uzalishaji mali na kuongeza kipato cha kaya.

“Mazingira ya jikoni yanakuwa safi zaidi kwa sababu hakuna moshi mkubwa unaozalishwa hii inasaidia kulinda afya za watumiaji huku ikitoa nafasi kwa wananchi kutumia muda wao katika shughuli nyingine za maendeleo,” alisema.

Akizungumzia changamoto ya baadhi ya wananchi kuendelea kuamini kuwa kuni ndiyo suluhisho pekee la nishati ya kupikia, alisema bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu ili kubadili mitazamo hiyo.



“Wananchi wengi wamezoea matumizi ya kuni kwa muda mrefu, lakini tunawaeleza kuwa dunia inabadilika na teknolojia za nishati safi zimekuja kutoa suluhisho bora zaidi. Faida zake ni nyingi kuanzia afya, mazingira hadi uchumi wa familia,” alisema.

Aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, upatikanaji wa maji na maisha ya wananchi kwa ujumla.



Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kuendelea kushirikiana katika kampeni za uhamasishaji ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata elimu na fursa ya kutumia nishati safi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



Akizungumza kuhusu shughuli za kampuni hiyo katika kongamano la nishati lililofunguliwa na Naibu waziri wa Nishati,Salome Nakamba jijini Arusha, Meneja Masoko wa Hanny G Investment, Zera Negro, amesema kampuni imejikita katika utengenezaji wa majiko ya kisasa yanayotumia umeme, gesi na briquettes zinazotokana na mabaki ya mazao ya kilimo, kwa lengo la kutoa suluhisho endelevu la nishati kwa taasisi na kaya.

Alisema  kampuni ya Hanny G Investment yenye makao yake Kiseliani-Moshono katika Jiji la Arusha imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, ambapo imefanikiwa kuzifikia taasisi zaidi ya 700 kupitia huduma zake za uzalishaji na usambazaji wa majiko pamoja na nishati mbadala ya kupikia.

Amesema mafanikio ya kampuni hiyo yameiwezesha kufikia taasisi zaidi ya 700 nchini zikiwemo shule, hospitali, magereza, vyuo, taasisi za kidini na ofisi mbalimbali zinazohudumia idadi kubwa ya wananchi kila siku.

“Tunajivunia kuona kuwa kupitia kampeni za uhamasishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia, tumefanikiwa kuzifikia taasisi zaidi ya 700 nchini. Hii ni hatua kubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema Zera.

Ameeleza kuwa kampuni hiyo imewekeza katika teknolojia za kisasa zinazosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, huku zikilinda afya za watumiaji na mazingira.

Kwa mujibu wa Zera, briquettes zinazozalishwa na Hanny G Investment hutengenezwa kutokana na mabaki ya mazao ya kilimo yanayopatikana ndani ya nchi, jambo linalosaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na wakati huo huo kupunguza utegemezi wa rasilimali za misitu.

Amesema mbali na kusambaza bidhaa zake, kampuni imekuwa ikitoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa taasisi mbalimbali nchini, huku ikifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha wateja wanaendelea kunufaika na huduma hizo.




About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia