WAHANDISI TANROADS, TARURA WATAKIWA KUTUMIA MIFUMO MIPYA KULINDA BARABARA
Ampongeza Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha barabara nchini
Na Mwandishi Wetu, Mbeya.
SERIKALI imewagiza mameneja na wahandisi wa TANROADS na TARURA nchini kutumia mifumo mipya ya kielektroniki kulinda hifadhi za barabara na kutekeleza miradi kwa viwango.
Agizo hilo limetolewa Jijini Mbeya Leo Juni 17 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Beno Malisa, kufungua mafunzo ya viongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Mafunzo hayo ya siku nne yaliyoanza Jumatatu, Juni 15, 2026, yamewakutanisha Mameneja, Wahasibu, na Wahandisi kutoka mikoa ya kimkakati ya kiuchumi ikiwemo Mbeya, Songwe, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, na Lindi.
Teknolojia na Udhibiti wa Miundombinu
Mhe. Itunda amebainisha kuwa lengo kuu la semina hiyo ni kuwajengea uwezo viongozi hao katika kusimamia miradi ya miundombinu kwa ufanisi, hasa kupitia matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki unaodhibiti na kusimamia matumizi holela ya hifadhi za barabara nchini.
Alitumia jukwaa hilo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumwaga mabilioni ya fedha katika ujenzi wa barabara, hatua iliyoleta mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi.
"Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa barabara zinajengwa na kuboreshwa ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi. Tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa juhudi hizi kubwa, na nitoe wito kwenu washiriki kutumia mafunzo haya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yenu," alisisitiza Mhe. Itunda.
Mapinduzi ya Kiuchumi vijijini
Pia, DC Itunda amewahimiza washiriki kutumia ipasavyo maarifa hayo ya kidijitali kuhakikisha utekelezaji wa miradi unazingatia viwango na taratibu zilizowekwa kiofisi bila kuwa na changamoto zozote.
Kitalamu, mafunzo haya yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili (TANROADS na TARURA), kuongeza uwajibikaji, na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa za kilimo na biashara katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na taifa kwa ujumla.

.jpeg)
.jpeg)

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia