CCM YATAKIWA KUEPUKA MAANDAMANO, KULINDA AMANI NCHINI
MAANDAMANO SI SULUHU, CCM WAONYWA
Na Woinde Shizza, Arusha
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Arusha, Ally Mwinyimvua maarufu kwa jina la Ally Meku, amewataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi kwa ujumla kujiepusha na maandamano yanayodaiwa kuitishwa kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa amani na usalama wa nchi vinapaswa kupewa kipaumbele wakati wote.
Meku alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi sita katika Kata ya Osunyai wilayani Arusha, ambapo alisema maandamano na vurugu za kisiasa mara nyingi huacha maumivu kwa wananchi wasiokuwa na hatia.
Alisema uzoefu wa matukio yaliyopita unaonyesha kuwa migogoro ya kisiasa inaweza kusababisha vifo, majeraha na hasara mbalimbali kwa wananchi, hivyo kuna haja ya kuchukua tahadhari na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.
Meku alisema bado anakumbuka matukio ya vurugu yaliyoripotiwa wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, ambapo baadhi ya wananchi walipoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa katika mazingira yaliyozua sintofahamu.
"Tuna wajibu wa kulinda amani na usalama wa nchi yetu. Tusikubali kurudia makosa yaliyopita ambayo yaliwaathiri wananchi wengi wasiokuwa na hatia," alisema.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujifunza kutokana na matukio hayo na kuepuka kushiriki mikusanyiko au maandamano yanayoweza kusababisha machafuko, hasa pale ambapo mazingira ya usalama hayajahakikishwa.
Kwa mujibu wa Meku, maendeleo ya taifa yanahitaji utulivu na mshikamano wa wananchi, akieleza kuwa amani ndiyo msingi muhimu wa utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika jamii.
Aidha, aliwataka wanachama wa CCM katika Kata ya Osunyai na maeneo mengine kuendelea kushiriki shughuli za maendeleo na kuunga mkono juhudi za serikali badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.
Meku alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kulinda umoja wa kitaifa na kuheshimu sheria za nchi ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na yenye mazingira rafiki kwa maendeleo
Naye Diwani wa Kata ya Osunyai, Elirehema Nnko, alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM unaendelea kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali za maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushirikiana katika kudumisha amani na utulivu.
.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia