MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA YATOA WITO WA ULINZI NA USTAWI WA WATOTO
Na Woinde Shizza,Arusha
Wadau wa maendeleo ya watoto, viongozi wa Serikali, wazazi na walezi wamehimizwa kuendelea kushirikiana katika kulinda haki na ustawi wa watoto ili kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kukua na kufikia ndoto zao.
Wito huo umetolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Viwanja vya Ngarenaro jijini Arusha, yakilenga kuwakumbusha wadau mbalimbali umuhimu wa kulinda haki, ustawi na maendeleo ya watoto barani Afrika.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Bi. Chausiku Baha, aliwataka wazazi na walezi kusimamia matumizi ya teknolojia kwa watoto, hususan simu za mkononi, ili kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya kujifunza na kuchochea maendeleo yao badala ya kuwa chanzo cha athari mbalimbali.
Alisema maendeleo ya teknolojia yameleta fursa nyingi kwa watoto katika kupata elimu na maarifa, lakini yanahitaji usimamizi wa karibu kutoka kwa wazazi na walezi ili kuwalinda dhidi ya matumizi mabaya yanayoweza kuathiri ukuaji wao.
Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya watoto, ambapo walijadili changamoto na fursa zilizopo katika kuhakikisha watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu, afya, ulinzi na malezi bora.
Washiriki walisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi za pamoja katika kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto pamoja na kuhakikisha kila mtoto anapata mazingira salama ya kujifunza na kuendeleza vipaji vyake.
Aidha, maadhimisho hayo yalitoa fursa kwa watoto kutoka maeneo mbalimbali ya Arusha kushiriki shughuli za kijamii na elimu zilizolenga kuwajengea uelewa kuhusu haki zao na wajibu wao katika jamii.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ilijikita katika kuimarisha ulinzi wa mtoto na kuhakikisha sauti za watoto zinasikika katika masuala yanayohusu maisha na maendeleo yao.
About Woinde Shizza
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia