PROGRAMU YA TAKUKURU RAFIKI YATAMBULISHWA KWA MADIWANI WA JIJI LA ARUSHA.
Na Woinde Shizza,Arusha
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imeitambulisha rasmi programu ya “TAKUKURU Rafiki” kwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika vita dhidi ya rushwa na kuhakikisha huduma za jamii pamoja na miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na uwazi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema lengo kuu la programu hiyo ni kupanua ushiriki wa wananchi na viongozi katika kuzuia na kupambana na rushwa kwa kubaini, kuchambua na kutatua changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za jamii na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema programu hiyo inalenga sekta muhimu zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, zikiwemo maji, elimu, afya, nishati ya umeme, barabara na ardhi Kwa mujibu wake, kubaini mapema changamoto na mianya ya rushwa katika sekta hizo kutasaidia kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ngailo amewataka madiwani kuwa mabalozi wa programu hiyo katika kata zao kwa kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU ili kuhakikisha malalamiko na kero za wananchi zinashughulikiwa kwa wakati, huku miradi ya maendeleo ikitekelezwa kwa kuzingatia matumizi sahihi ya rasilimali za umma.
Baadhi ya madiwani waliohudhuria kikao hicho wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yatawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika kusimamia maendeleo ya wananchi.
Diwani wa Kata ya Kimandolu amesema semina hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu nafasi yao katika kuzuia rushwa na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akiomba ushirikiano wa karibu zaidi kati ya TAKUKURU na viongozi wa kata ili kutatua changamoto za wananchi kwa haraka.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Themi, Mellance Kinabo, amesema programu ya TAKUKURU Rafiki itasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya taasisi hiyo na wananchi kupitia viongozi wao, jambo litakalorahisisha uibukaji wa taarifa za changamoto zinazokwamisha maendeleo katika jamii.
Ameongeza kuwa programu hiyo itasaidia pia kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na kuhakikisha rasilimali zinazotolewa na Serikali zinawafikia walengwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Programu ya TAKUKURU Rafiki inatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika kulinda rasilimali za umma na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Arusha.















0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia