EU, SERIKALI YAJIVUNIA MAFANIKIO YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Na Woinde Shizza, Arusha
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania na Naibu Waziri wa Nishati wamejivunia mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia nchini, huku kiwango cha matumizi ya nishati hiyo kikiongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa nishati safi ya kupikia uliofanyika jijini Arusha, Balozi wa Umoja wa Ulaya EU Christine Grau alisema EU imetoa zaidi ya Sh bilioni 92 kupitia Cook Fund, ruzuku ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kutolewa na umoja huo kwa sekta ya nishati safi ya kupikia katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alisema fedha hizo zimewezesha zaidi ya kaya 482,000 zenye wanufaika zaidi ya watu milioni 2.2 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza kupata huduma za nishati safi ya kupikia.
Alisema kupitia Cook Fund inayotekelezwa kwa ushirikiano na UNCDF, zaidi ya ruzuku 102 zimetolewa kwa biashara ndogo na za kati huku takribani biashara 5,000 zikifaidika.
Aidha, shule na taasisi 145 zinatarajiwa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua ambayo imechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia, kupunguza matumizi ya kuni na kuwapa wanafunzi muda zaidi wa masomo.
Balozi huyo alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia mashuleni yameleta manufaa makubwa kwa wanafunzi kwa kuwa yanapunguza muda uliokuwa ukitumika kutafuta kuni na kushughulikia shughuli za upishi.
Alisema hali hiyo imechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika baadhi ya shule zilizonufaika na mpango huo.
Aidha, alisema Umoja wa Ulaya umeendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira kupitia programu za misitu na uendelevu zinazotekelezwa kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali, hatua ambayo imechangia kupunguza kasi ya ukataji miti na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za misitu nchini.
Akihitimisha hotuba yake, Balozi wa Umoja wa Ulaya alisema ingawa Cook Fund itafikia mwisho wake Septemba 2026, EU itaendelea kushirikiana na Tanzania katika juhudi za kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Tumeshuhudia jinsi ruzuku hii ilivyobadilika kutoka kuwa mradi wa kawaida hadi kuwa harakati kubwa yenye matokeo chanya kwa jamii ,sisi tumesaidia kufungua ukurasa, lakini wadau wa Tanzania ndio wanaoandika historia kamili ya mafanikio haya,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati alisema matumizi ya kuni na mkaa kwa muda mrefu yamekuwa yakisababisha madhara kwa afya za wananchi, hususani wanawake na watoto, pamoja na kuharibu misitu na kuongeza gharama za kijamii na kiuchumi, na kubainisha kutokana na hali hiyo, Serikali imeifanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa moja ya vipaumbele vya Taifa.
Alisema kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, akibainisha kuwa ongezeko la matumizi kutoka asilimia 6.9 hadi 28.6 ndani ya miaka michache linaonyesha kuwa lengo hilo linawezekana kufikiwa iwapo jitihada za sasa zitaendelezwa.
Naibu Waziri huyo alisema mafanikio hayo yametokana na usambazaji wa mitungi ya gesi ya LPG kwa bei nafuu, matumizi ya majiko banifu, miradi ya biogas, matumizi ya umeme kwa kupikia pamoja na kampeni za elimu kwa umma zinazotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu faida za nishati safi.
Aliongeza kuwa kupitia Cook Fund, zaidi ya dola za Marekani milioni 10.1 sawa na Sh bilioni 26.5 zimetolewa kwa biashara ndogo na za kati 102, huku zaidi ya kaya 634,000 na wanafunzi zaidi ya 72,000 wakinufaika na huduma za nishati safi ya kupikia kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa nchini.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia