KIHONGOSI KUTINGA ARUSHA, WANANCHI WATAKIWA KUWASILISHA KERO ZAO

 




Na  Woinde Shizza, Arusha

Wananchi wa Mkoa wa Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara itakayofanyika wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, ili kuwasilisha kero, changamoto na maoni yao kwa viongozi wa chama na serikali.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Saipulani Ramsey, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ziara ya siku tatu ya Kihongosi inayotarajiwa kuanza Juni 4 hadi 6 mwaka huu.

Ramsey amesema ziara hiyo inalenga kuwasogezea wananchi viongozi wa chama na serikali ili kusikiliza changamoto zao na kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayowagusa katika maisha ya kila siku.

Amesema pamoja na kusikiliza kero za wananchi, Kihongosi na ujumbe wake watapata fursa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

Kwa mujibu wa Ramsey, wananchi watapata nafasi ya kutoa maoni kuhusu mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa na serikali.

Aidha, sehemu ya ziara hiyo itahusisha kukagua uhai wa chama katika ngazi mbalimbali kuanzia matawi, kata, wilaya hadi mkoa kwa lengo la kuimarisha CCM na kuongeza ushiriki wa wanachama katika shughuli za kisiasa na maendeleo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Kihongosi ataanza ziara yake Wilaya ya Karatu Juni 4, kabla ya kuendelea Wilaya ya Arumeru Juni 5 na kuhitimisha ziara hiyo kwa mkutano mkubwa wa hadhara katika Jiji la Arusha Juni 6.



Wakati huo huo, CCM Mkoa wa Arusha imesema imefanikiwa kufika katika kata 107 kati ya kata 161 zilizopo mkoani humo kupitia ziara ya awamu ya pili ya kuimarisha chama inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya.

Ramsey amesema ziara hizo zimekuwa daraja muhimu la kuunganisha wananchi na viongozi wa chama kwa kuwa zimewezesha wananchi kueleza changamoto zao moja kwa moja huku chama kikijipatia mrejesho wa maendeleo na huduma zinazotolewa katika maeneo mbalimbali.

Amesema CCM itaendelea kuwafuata wananchi walipo, kusikiliza maoni yao na kushirikiana na serikali kutatua changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla.









About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia