CHONGOLO: MIRADI YA SAMIA INABADILISHA SURA YA ARUSHA, AFCON 2027 NI FURSA YA UCHUMI
CHONGOLO: MIRADI YA SAMIA INABADILISHA SURA YA ARUSHA, AFCON 2027 NI FURSA YA UCHUMI
Na Woinde Shizza, Arusha
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi katika Wilaya ya Arusha, Chongolo alikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Bondeni City kinachojengwa katika Kata ya Olmot kwa gharama ya Sh bilioni 14.3, fedha zilizotolewa na Serikali.
Alimshukuru Rais Samia kwa kuridhia fedha za mradi huo, akisema stendi hiyo itakapokamilika itaondoa msongamano wa magari katikati ya jiji, kuboresha huduma za usafiri na kufungua fursa mpya za biashara, ajira na uwekezaji kwa wananchi wa Arusha.
Chongolo alisema uamuzi wa kujenga stendi hiyo nje ya katikati ya jiji umezingatia mipango ya maendeleo ya muda mrefu, akieleza kuwa eneo hilo limeunganishwa na barabara muhimu ikiwemo Ring Road na barabara zinazounganisha mikoa na wilaya mbalimbali.
"Baada ya miaka miwili mtatambua kuwa eneo hili ndilo litakuwa kitovu kipya cha Jiji la Arusha kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea," alisema.
Katika ziara hiyo, Waziri huyo pia alikagua mradi wa ujenzi wa Uwanja wa AFCON 2027 na kueleza kuwa maandalizi yanayoendelea yanaonyesha utayari wa Tanzania, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, kuwa wenyeji wa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Alisema ujenzi wa uwanja huo umefungua ajira kwa vijana wengi na kuharakisha maendeleo ya miundombinu, huku akiwahimiza wananchi kujiandaa kutumia fursa zitakazotokana na ongezeko la wageni, biashara na uwekezaji wakati wa mashindano hayo.
Kwa upande mwingine, Chongolo aliwataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu, akieleza kuwa Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya shule na kutoa elimu bila malipo ili kila mtoto wa Kitanzania aweze kutimiza ndoto zake.
Waziri huyo alitoa wito huo baada ya kuzindua nyumba ya walimu yenye familia mbili (2 in 1) katika Shule ya Sekondari Kalimaji, Kata ya Moshono, iliyojengwa kwa gharama ya Sh milioni 130 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Aidha, aliagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk. Toba Alnason Nguvila, kufanyia kazi ombi la kupandisha hadhi Shule ya Sekondari Kalimaji ili ianze kutoa elimu ya kidato cha tano na sita, huku akipongeza viongozi wa mkoa na halmashauri kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi.
















0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia