HUDUMA ZA MATIBABU BILA MALIPO ZAANZA RASMI ARUSHA
Wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo mbalimbali nchini wameanza kupatiwa huduma za matibabu ya kibingwa bila malipo katika Kambi ya Matibabu ya Arusha Afya Plus, inayoendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kabla ya kuanza kwa huduma hizo, Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb), aliongoza maombi maalumu ya kuliombea tukio hilo, dawa, vifaa tiba pamoja na madaktari na wataalamu wa afya wanaotoa huduma.
Akizungumza na madaktari, wauguzi na wataalamu wa afya, Mhe. Makonda alisema pamoja na maandalizi yote ya kitaalamu, mafanikio ya huduma hizo yanahitaji pia baraka za Mungu.
“Tunazo dawa, tunao madaktari bingwa na vifaa vya kisasa, lakini tunahitaji pia mkono wa Mungu. Tunaomba kila atakayepokea dawa na matibabu haya apate uponyaji na awe ushuhuda wa wema wa Mungu,” amesema Makonda.
Siku ya kwanza ya kambi hiyo imeanza kwa mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kupima afya na kupata huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo magonjwa ya moyo, kisukari, saratani, macho, afya ya uzazi, mifupa, magonjwa ya ndani na huduma nyingine za kibingwa.
Kambi hiyo itaendelea kwa siku saba ikiwa na lengo la kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kuhamasisha utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mapema na kuboresha afya za Watanzania.
#PaulMakonda #ArushaMjini #ArushaAfyaPlus #KambiYaMatibabu #AfyaBoraTaifaImara #MatibabuBure #Arusha #Tanzania 🏥🇹🇿

























0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia