MRADI WA KUKU WA MAYAI WA SH. MILIONI 200 WANG'ARA MBIO ZA MWENGE ARUSHA



Na Woinde Shizza, Arusha

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Michael Mwang'onda, ametembelea na kukagua mradi wa ufugaji wa kuku wa mayai wa Dalv Products uliopo Kata ya Osunyai, Arusha, ukiwa miongoni mwa miradi inayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula, ajira na kukuza uchumi wa wananchi.


Mradi huo unaomilikiwa na mkurugenzi Veronica Aloyce Tarimo, ulianzishwa mwaka 2008 ukiwa na kuku 400, lakini sasa umekua na kufikia kuku wa mayai 5,000, huku ukiwa na lengo la kufikia kuku 15,000 mara utakapokamilika.


Akitoa taarifa ya mradi huo, Tarimo alisema uwekezaji huo wenye thamani ya Shilingi milioni 200 umehusisha ununuzi wa ardhi, ujenzi wa mabanda, mashine za kutengeneza chakula cha kuku, malighafi, battery cages, vifaranga, vifaa mbalimbali pamoja na dawa.



Alisema kwa sasa mradi huzalisha wastani wa trei 150 za mayai kwa siku, huku soko lake likiwa ni makampuni, hoteli za kitalii pamoja na maduka makubwa ya bidhaa (supermarkets).


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi huo umechangia kutoa ajira za moja kwa moja kwa vijana watano, huku pia ukinufaisha familia na jamii kupitia shughuli za uzalishaji na biashara zinazotokana na ufugaji wa kuku.


Aidha, Tarimo alisema mradi umeweka kipaumbele katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati ya biogas inayozalishwa kutokana na kinyesi cha kuku, hatua inayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na matumizi ya nishati nyingine.



Alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, hali inayowawezesha wawekezaji kuanzisha na kupanua miradi ya maendeleo.



Mwenge wa Uhuru unaendelea kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Arusha kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji, uwajibikaji na maendeleo ya wananchi.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia