MWENGE WA UHURU WAKAMILISHA UKAGUZI WA MIRADI YA SH. BILIONI 3.9 ARUSHA
Mwenge wa Uhuru 2026 umekamilisha mbio zake katika Jiji la Arusha baada ya kutembelea na kukagua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.9, huku ukihimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuendeleza miradi hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mwenge huo ulikimbizwa umbali wa kilometa 89.2 ukipitia maeneo mbalimbali ya jiji, ambapo ulitembelea miradi inayotekelezwa katika sekta za maji, afya, elimu, miundombinu, mazingira na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni tenki la maji la Kimindorosi lililopo Olasiti, ambalo linatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo, pamoja na mradi wa mazingira na matumizi ya nishati safi katika Shule ya Sekondari Arusha.
Katika sekta ya elimu, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alitembelea Shule ya Sekondari Muriet iliyopo Bondeni City, ambako alikagua maboresho ya miundombinu yaliyolenga kuinua ubora wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Kwa upande wa afya, Mwenge ulikagua jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Moivaro, mradi unaotarajiwa kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo jirani.
Aidha, Mwenge ulitembelea Barabara ya Ugiriki iliyojengwa kuboresha miundombinu ya usafiri, pamoja na kukagua miradi ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ikiwemo Kikundi cha Vijana cha Mclives Limited na mradi wa ufugaji wa kuku wa Devi uliopo Osunyai.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Modest Mkude, alisema Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chachu ya maendeleo kwa kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kusimamia na kulinda miradi inayotekelezwa na Serikali.
"Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo cha kuhamasisha wananchi kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu. Miradi yote iliyotembelewa inalenga kuboresha maisha ya wananchi na kuonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi," alisema Mkude.
Aliongeza kuwa mafanikio ya miradi hiyo yatategemea ushirikiano kati ya Serikali na wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuitunza ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.
Mbali na ukaguzi wa miradi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru alitoa elimu kwa wananchi kuhusu lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, kinga dhidi ya malaria pamoja na maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Mwenge wa Uhuru uliondoka Arusha ukiwa umeacha ujumbe wa uzalendo, uwajibikaji na mshikamano kwa wananchi, sambamba na kaulimbiu ya mwaka 2026 isemayo, "Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo," inayohimiza kila Mtanzania kushiriki katika kuijenga na kuiendeleza nchi.








0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia