JKCI YAANZISHA MFUMO WA KIDIJITALI WA KUFUATILIA WAGONJWA HADI WAKIWA NYUMBANI
JKCI YAANZISHA MFUMO WA KIDIJITALI WA KUFUATILIA WAGONJWA HADI WAKIWA NYUMBANI
Na Woinde Shizza, Arusha
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imezindua mfumo wa kisasa wa kidijitali wa usajili na ufuatiliaji wa wagonjwa kwa kutumia teknolojia ya Dozee, unaowezesha madaktari kufuatilia hali ya wagonjwa kwa wakati halisi hata wanapokuwa majumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika jijini Arusha, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Christian Makonda, aliyesema hatua hiyo inaonesha namna Tanzania inavyoendelea kutumia teknolojia kuboresha huduma za afya na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Makonda alisema matumizi ya teknolojia katika usajili na ufuatiliaji wa wagonjwa yatasaidia kupunguza urasimu, kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za matibabu nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, alisema mfumo wa Dozee hutumia kifaa maalumu kisichohitaji kuunganishwa moja kwa moja na mwili wa mgonjwa, bali hufuatilia viashiria muhimu vya afya kama mapigo ya moyo, kiwango cha oksijeni kwenye damu, shinikizo la damu pamoja na viashiria vingine muhimu.
Alisema taarifa zote hukusanywa na kutumwa kwa njia ya kidijitali, hivyo madaktari wanaweza kuona mwenendo wa afya ya mgonjwa kupitia simu au kompyuta bila kumlazimu mgonjwa kufika hospitalini mara kwa mara.
Dkt. Kisenge alieleza kuwa teknolojia hiyo inalenga kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vinavyotokana na wagonjwa kubadilika hali ghafla wakiwa majumbani baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
"Mara nyingi wagonjwa wanaporuhusiwa kurudi nyumbani hali zao zinaweza kubadilika ghafla. Kupitia mfumo huu, madaktari watapata taarifa mapema na kuchukua hatua kabla hali haijawa mbaya," alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa mfumo huo ni sehemu ya jitihada za JKCI kuendelea kutumia ubunifu na teknolojia katika kuboresha huduma za afya, kuongeza usalama wa wagonjwa na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa ufanisi zaidi ndani na nje ya hospitali.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia