TCRA YATOA AHUENI KWA BLOGA, WANAMITANDAO

Na Woinde Shizza, Dodoma


Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa nafuu kwa waandishi wa habari na wananchi wanaoanzisha mitandao ya habari kwa mara ya kwanza, kwa kuondoa ada ya mwaka mmoja wa leseni, hatua ambayo imelenga kuhamasisha ubunifu na kukuza sekta ya mawasiliano nchini.


Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji uliofanyika Februari 12, 2026 jijini Dodoma, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alisema waandishi watakaonufaika na mpango huo watajulikana kama Amateur (wanaoanza) na hawatalazimika kulipa ada ya mwaka wa kwanza.


Mhandisi Kisaka alieleza kuwa uamuzi huo umetokana na mapendekezo yaliyotolewa kupitia utafiti wa huduma za utangazaji nchini, ambao ulionesha changamoto zinazowakabili wanahabari wachanga na wabunifu wanaotaka kuanzisha majukwaa ya kidijitali.


“Tumeona ni busara kutoa ahueni hii ili kuwapa nafasi waandishi na wabunifu kujifunza, kujenga uzoefu na kuboresha ubora wa kazi zao kabla ya kuingia katika mfumo rasmi wa leseni,” alisema Kisaka.


Awali, mwanzilishi wa mtandao wa habari alitakiwa kulipa Sh. 50,000 kama ada ya maombi na Sh. 500,000 kama ada ya leseni ya mwaka, kiasi ambacho kilionekana kuwa kikwazo kwa vijana wengi wanaotaka kuanzisha majukwaa ya habari mtandaoni.

Aidha alisema kuwa kwa sasa mwanzilishi wa mtandao wa habari anatakiwa kulipa ada ya maombi ya leseni shilingi elfu kumi na ada ya leseni kwa mwaka sh.100000 kiasi ambacho kitamuwezesha  kijana kuweza kulipa ada na kuendesha chombo cha habari kwa leseni

Tangazo hilo lilipokelewa kwa shangwe na makofi kutoka kwa washiriki wa mkutano huo, ambao wengi wao ni wamiliki wa mitandao ya kijamii na wanachama wa vyama vinavyosimamia tasnia hiyo.


Miongoni mwa waliokuwepo ni wanachama wa Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN), Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), NIBA, Wakongwe RTD, Baraza la Habari Tanzania (MCT) na MISA-TAN.


Washiriki hao wamesema hatua hiyo ya TCRA ni mwanzo mzuri wa kuimarisha mazingira rafiki kwa uandishi wa habari mtandaoni na kuchochea ukuaji wa sekta ya habari za kidijitali nchini.












About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia