DKT. MWIGULU AFURAHISHWA NA MABADILIKO MAKUBWA ARUSHA

 




Na Woinde Shizza, Arusha


WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo jijini Arusha, ikiwemo ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Bondeni City Bus Terminal na Soko la Kilombero, akisisitiza uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara kwa wananchi.


Akizungumza Februari 24, 2026, katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Soko la Kilombero, Dkt. Nchemba alisema kukamilika kwa stendi mpya ya mabasi inayojengwa katika Kata ya Murrieth kutapunguza msongamano wa magari, kupanua huduma za usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi jijini humo.


“Stendi ya sasa ni finyu na imebana sana ,Mradi huu mpya utaongeza nafasi, kuboresha huduma na kufungua fursa zaidi za kibiashara kwa wananchi,” alisema Waziri Mkuu.


Katika kuimarisha miundombinu ya jiji, alielekeza barabara muhimu zijengwe kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa mijini.


Mradi wa Soko la Kilombero, unaotekelezwa na kampuni ya Mohammed Builders Limited kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.5, ulianza Mei 30, 2025 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2026. Hadi sasa umefikia asilimia 66 ya utekelezaji, ambapo mkandarasi amelipwa Shilingi bilioni 3.95, sawa na asilimia 41.66 ya gharama zote.


Kwa mujibu wa maelezo ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, soko hilo lina vizimba 518 vinavyoweza kuhudumia wafanyabiashara 2,072 kwa wakati mmoja, maliwato ya kisasa kwa jinsia zote, wazee na watu wenye ulemavu, kituo cha polisi, ofisi ya zimamoto, chumba cha huduma ya kwanza, na bustani ya mapumziko pamoja na maegesho ya magari, malori, bodaboda na bajaji.


Aidha, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo, kuongeza idadi ya masoko rasmi ili kuwapa wafanyabiashara maeneo bora, salama na yenye wateja wa uhakika.


Alisisitiza kuwa wafanyabiashara waliopisha eneo la mradi wa Kilombero watapewa kipaumbele katika ugawaji wa maduka, huku akionya dhidi ya vitendo vya ulanguzi, upendeleo na wizi.


“Nataka haki itendeke fanyeni sensa kubaini wahusika halali ,Mtumishi wa umma atakayebainika kujimiliki duka kinyume cha utaratibu atachukuliwa hatua kali,” alionya.



Mradi wa Bondeni City Bus Terminal, unaotekelezwa sambamba na Soko la Kilombero, unajumuisha miundombinu ya kisasa yenye maegesho ya magari, maeneo ya kupakia na kushusha abiria, mifumo ya usalama na huduma za mizigo.


Miradi hii inatekelezwa chini ya mpango wa TACTIC kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara, ajira na mapato ya Halmashauri.



Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo inalenga kuongeza kasi ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia