WAZIRI DKT. GWAJIMA AITAKA SEKRETARIETI YA MTAKUWWA KUONGEZA KASI, USHIRIKIANO NA URATIBU KATIKA KUTOKOMEZA UKATILI
Na WMJJWM - Arusha
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), ameitaka Sekretarieti ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kuimarisha uwajibikaji, ushirikiano na uratibu katika utekelezaji wa majukumu yake ili kufanikisha malengo ya mpango huo. Waziri Gwajima ametoa msisitizo huo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Sekretarieti ya MTAKUWWA kilichofanyika Februari 11, 2026 jijini Arusha.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Gwajima amesema Sekretarieti ndiyo mhimili wa MTAKUWWA kwa kuwa ndiyo inasimamia utekelezaji wa shughuli za kila siku za mpango huo ikiwemo uandishi wa taarifa za utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya afua, pamoja na uratibu wa wadau huku akiwataka wajumbe wa Sekretarieti kujitoa kwa dhati, kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha jamii inafikiwa kwa afua zitakazosaidia kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Waziri Gwajima amebainisha kuwa kikao hicho kina jukumu la kukamilisha taarifa ya utekelezaji wa MTAKUWWA kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, kuandaa mpango wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2026/27 pamoja na kukamilisha dodoso la kielektroniki la ukusanyaji wa taarifa. Alieleza kuwa maandalizi hayo ni muhimu kwa kuwa taarifa hizo zitawasilishwa katika ngazi za juu za maamuzi ikiwemo Kamati ya Makatibu Wakuu na Baraza la Mawaziri.
Kabla ya kuhitimisha hotuba yake, Mhe. Gwajima aliwakumbusha washiriki mambo matatu muhimu ya kuzingatia ambayo ni uwajibikaji katika utekelezaji na utoaji wa taarifa kwa wakati, kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu, pamoja na kuimarisha uratibu wa afua ili kuepuka migongano na upotevu wa rasilimali. Aliwataka washiriki kutumia kikao hicho kama jukwaa la kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa lengo la kuimarisha ulinzi, usalama na ustawi wa wanawake na watoto nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Sera, Utafiti na Ubunifu, Ally Nunduma, akizungumza kwa niaba ya Sekretarieti, amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi kikamilifu.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia