WAANDISHI WAHIMIZWA KUPAMBANA NA TAARIFA POTOFU
Na Mwandishi wetu - Geita
Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, amesema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi badala ya taarifa potofu, akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya upotoshaji wa habari yanahitaji weledi, maadili na matumizi sahihi ya teknolojia.
Akifungua mafunzo maalum kwa waandishi wa habari Mkoa wa Geita kuhusu Uthibitishaji na Uhakiki wa Taarifa yaliyofanyika Jumatano, Februari 18, 2026 mjini Geita, Simbaya amesema katika dunia ya sasa yenye wingi wa taarifa, ni rahisi kwa jamii kupotoshwa iwapo waandishi hawatakuwa makini katika uchambuzi na uthibitishaji wa habari.
“Wananchi wanahitaji taarifa sahihi zitakazowasaidia kufanya maamuzi sahihi. Jukumu la mwandishi ni kuhakikisha jamii inapata ukweli. Ndiyo maana tumeona umuhimu wa kuandaa mafunzo haya. Nendeni mkatumie elimu hii kwa vitendo. Tunataka muandike habari zenye uwezo wa kubadili jamii na kujenga taifa,” amesema Simbaya.
Ameongeza kuwa UTPC inataka kuona waandishi wakiendelea kushikilia misingi ya maadili ya taaluma yao na kuandika habari zenye tija zisizopotosha umma.
Lengo kuu ni kuwajengea waandishi uwezo wa kukabiliana na changamoto za fake news, misinformation na disinformation ambazo zimekuwa tishio kubwa duniani.
Washiriki wamepatiwa mbinu mbalimbali za uthibitishaji wa habari, ikiwemo matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), kugundua asili ya picha na video, kulinganisha taarifa na vyanzo vinavyoaminika, pamoja na kusoma zaidi ya vichwa vya habari ili kuepuka kupotoshwa.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa “Ukweli Kwanza” unaolenga kuongeza weledi wa waandishi wa habari na kuimarisha uwezo wa wananchi kupambana na upotoshaji wa taarifa. Kupitia mradi huo, waandishi wanafundishwa mbinu za fact-checking, matumizi sahihi ya teknolojia na namna ya kutambua na kukabiliana na misinformation na disinformation.
Aidha, mradi huo unalenga kuwawezesha waandishi chipukizi, hususan wanawake, kuwa mstari wa mbele katika kulinda ukweli na kuimarisha uaminifu wa vyombo vya habari nchini.
Kupitia mafunzo haya, UTPC na wadau wake wanaamini kuwa waandishi wa habari wataendelea kuwa nguzo muhimu ya ukweli, uwazi na uwajibikaji katika jamii.
Kupitia mafunzo haya, UTPC na wadau wake wanaamini kuwa waandishi wa habari wataendelea kuwa nguzo muhimu ya ukweli, uwazi na uwajibikaji katika jamii.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi.






0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia