Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Afungua Mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira

 



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba Afungua Mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira
Ngurudoto, Arusha – Februari 24, 2026 –

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amefungua rasmi mkutano wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika hoteli ya Ngurudoto, Arusha, akisisitiza umuhimu wa kutoa huduma ya maji kwa wananchi bila ucheleweshaji.



Akieleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema serikali imekwamua miradi iliyoshindwa kutekelezwa kwa muda mrefu na kuanzisha miradi mipya katika maeneo yaliyoathirika na uhaba wa maji.

“Tunatakiwa tushinde ‘Site’, pale ambapo fedha ipo na wananchi wanahitaji maji. Hatutakiwi kuchelewesha hata kwa nusu saa maji ambayo yalitakiwa yameshapatikana. Kupanga maisha bila maji ni jambo gumu sana,” alisema Dkt. Nchemba.

Aidha, alisisitiza kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la kila Mtanzania. “Tukichezea vyanzo vya maji hata kama fedha zipo, tutakosa maji. Si jambo zuri kusikia wananchi wanakosa maji halafu kuna mahali maji yanapotea. Kagueni miundombinu yetu ya usambazaji wa maji ili tukomeshe upotevu wa maji,” alisema.

Waziri Mkuu pia alieleza kuwa kila mkoa umepatiwa mitambo ya kuchimba maji, na mamlaka za maji zinapaswa kutumia rasilimali zilizopo kuhakikisha wananchi wanapata maji. “Mkoa wowote ambao wananchi watalalamika kuhusu kukosa maji, mamlaka za maji zitakuwa zinalikwamisha hilo. Tunataka tuwape tabasamu Watanzania, maji hayana mbadala,” alisema.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa maji katika shule, zahanati na vituo vya afya. “Kila shule ya msingi na sekondari, zahanati, vituo vya afya viwe na maji. Mitambo tuliyo nayo tunapaswa kuhakikisha hili linafanikiwa,” alibainisha.

Dkt. Nchemba aliongeza kuwa utunzaji wa vyanzo vya maji ni jukumu la pamoja, sio la mamlaka za maji pekee, wala wizara ya Maji au Wizara ya Maliasili na Utalii pekee. “Tunatunza uhai wetu tunapotunza vyanzo vya maji,” alisema.

Katika hitimisho, alieleza kuridhishwa kwake na maendeleo yaliyopigwa katika sekta ya maji. “Tumeshapiga hatua kubwa sana katika kuwapa maji Watanzania, twendeni tukamalizie palipobaki,” alisema Dkt. Nchemba.




About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia