AMUUA SHEMEJI YAKE KWA SUMU

Kamanda wa polisi mkoa Arusha Thobias Andengenye akiongea na waandishi wa habari
 
Mkazi mmoja wa kijiji cha Pinyinyi wilayani Ngorongoro anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua shemeji yake kwa kumwekea sumu  kwenye pombe ya kienyeji .

Kamanda  wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema tukio hilo limetokea Mei 7 mwaka huu katika kijiji hicho wilayani Ngorongoro, ambapo  mtuhumiwa huyo aitwae,  Kumari Nangau, ambae ni mfugaji alimnunulia marehemu pombe kisha kuitia dawa inayoaminika kuwa sumu .

Alisema chanzo ni ugomvi uliotokea baina yao uliosababishwa na marehemu kudaiwa kwa muda mrefu  deni la shilingi 320,000, hatua iliyofuatiwa na mtuhumiwa kumchukua mke wa marehemu ambae ni mdogo wake na kumrudisha nyumbani kwao mpaka deni litakapolipwa.

Marehemu aliweza kulipa deni hilo na alitarajia kurudishiwa mke wake lakini wazazi wa mke walimkatalia binti yao kwa kutoridhishwa na tabia ya mume wake hatua iliyosababisha mtuhumiwa kujenga chuki na marehemu kuwa ndie aliyesababisha mke wake kuondoka na kutorejea nyumbani kwake.

Kamanda Andengenye, alisema kuwa mara baada ya marehemu kunywa pombe hiyo hali yake ilibadilika ghafla na kuomba maji ya kunywa ambapo watu aliokuwa nao walishauri mtu huyo apewe maziwa ila alifariki ghafla  alifariki kabla ya kunywa maziwa hayo.

Mara baada ya tukio hilo mtuhumiwa alijaribu kukimbia lakini alikamatwa na Askari mgambo ambao walimpeleka polisi ambako anashikiliwa akisubiri kufikishwa mahakamani .

Alisema kuwa uchunguzi uliofanywa na Daktari wa hospitali Teule ya wilaya ya Ngorongoro, umeonyesha kuwa marehemu alikunywa sumu ,lakini hata hivyo sampuli za vipimo zaidi zimepelekwa kwa Mkemia mkuu wa serikali .

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post