BREAKING NEWS

Friday, May 18, 2012

WANACHAMA 500 MANYARA WAAMIA CHADEMA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara (Chadema) Pauline Gekul
akihamasisha salamu ya chama hicho ya nguvu ya umma (Peoples Power) ya
kukunja ngumi na kunyoosha mkono juu kwa wananchi wa kijiji cha
Mwinkantsi kata ya Mamire kwenye ziara ya operesheni vua gamba vaa
gwanda ambapo mabalozi 70 na wanachama 26 wa CCM walijiunga Chadema

MBUNGE wa Viti maalum Mkoani Manyara (Chadema) Pauline Gekul
ameendesha operesheni vua gamba vaa gwanda wilayani Babati na
kufanikiwa kupata wanachama wapya zaidi ya 500 na mabalozi 240 wa CCM.

Katika operesheni hiyo ya vua gamba vaa gwanda iliyoanza wiki
iliyopita na kuendelea jana,ilihusisha Kata za
Magugu,Bohai,Bashnet,Gidas,Galapo,Mamire Endakiso na Mwikansi ambapo
kadi ya Tanu iliyotolewa 7/7/1976 ilirudishwa.

Akizungumza wakati akiwapokea wanachama hao,Gekul alisema viongozi wa
CCM wameshindwa kutatua kero,matatizo na changamoto zinazowakabili
wananchi hivyo wakati wa CCM kuwa chama cha upinzani umefika.

Alisema wananchi wamechoshwa na maisha magumu yaliyosababishwa na
viongozi wa CCM ikiwemo mfumuko wa bei hivyo ili kuepuka hali hiyo ni
kuiondoa CCM madarakani na kuiweka Chadema na ndiyo utakuwa ufumbuzi
wa maendeleo.

“Uchaguzi wowote wa Serikali za mitaa wa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu
wa 2015 tutaitoa CCM madarakani kwa sanduku la kura kwani hatutaitoa
CCM kwa kutumia mapanga,marungu au silaha yoyote,” alisema Gekul na
kuongeza;

“Mabalozi wameniambia walikuwa wanalipwa sh5,000 kipindi cha uchaguzi
sawa na kulipwa sh1,000 kila mwaka kwani wanasubiri hadi miaka mitano
ipite walipwe tena hivyo wamechoka na hayo na sasa wamehamia huku
kwetu”

Pia Gekul alijitolea sh500,000 kwa ajili ya kununua vifaa vya ofisi
ikiwemo viti na mafaili za vijiji na kata ambapo awali aliombwa
asaidie vifaa hivyo vya ofisi ambazo zitakuwa wazi muda wote kwa ajili
ya kusikiliza kero za jamii.

Naye,Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Babati,Meja Muhammad Madole
alisema wabunge wa CCM wamekuwa wagumu kuwatembelea wananchi ili
kubaini changamoto zinazowakabili.

“Ninyi baada ya kuwachagua hawakurudi kwenu kutoa hata shukrani hivi
sasa baada ya kuona sisi tunazunguka ndiyo wanaanza kuja mfano juzi
tulikuwa Gidas na jana mbunge wenu akaenda huko na leo tupo hapa kesho
naye atakuja,” alisema.

Aliwataka wakazi wa wilaya hiyo wajiandae kujitokeza kwa wingi kutoa
maoni yao baada ya Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya itakapofika
wilayani humo na pia wajitokeze kwa wingi kwenye zoezi la sensa ya
watu na makazi.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates