MONDULI WACHACHAMAA NA KATIBA MPYA




 Mwenyekiti wa UVCCM Monduli Juilus Kalanga
 WANANCHI wa Monduli wametakiwa kujitokeza kwenye mikutano ya kukusanya maoni ya katiba mpya ili waweze kutoa mapendekezo yatakayowawezesha kunufaika na rasilimali zao ikiwemo misitu na mapori yanayotumika kwa utalii wa kuwinda. Hayo yalisemwa na mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Julius Kalanga wakati alipokuwa akiwaeleza waandishi wa habari maazimio ya kikao cha kamati ya utekelezaji kilichokaa mwishoni mwa wiki .

 Alisema kuwa wilaya hiyo ina misitu na vitalu vya uwindaji wa kitalii lakini wananchi wake hawanufaiki navyo kwani malipo yote hufanyikia wizarani jambo alilosema kuwa si sahihi kwani wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo hayo ambao huwa walinzi na hupata athari mbalimbali ikiwemo wanyama kuvamia mashamba na makazi yao hivyo wanapaswa kupata sehemu ya mapato.

 Kalanga ambaye pia ni diwani wa Nyampulukano alisema kuwa tatizo hilo linaweza kutatuliwa kwa wananchi kujitokeza kwenye mikutano ya kukusanya maoni ya katiba mpya ambapo alishauri angalau asilimia 25 mpaka 30 ya mapato ya uwindaji wa kitalii na uvunaji wa miti kwa ajili ya mbao yakarudishwa kwa jamii zinazoishi kwenye maeneo kuzunguka vitalu vya uwindaji na mazao ya misitu.

 Aidha Mwenyekiti huyo wa UVCCM alisema kuwa wanamshukuru mbunge wao, Edward lowassa kwa kuamua kuweka wazi msimamo wake wa kutokihama chama hicho tawala kwani kabla ya hapo kulitokea sintofahamu kubwa miongoni mwa wanaCCM ambao wengine walitaka kukihama chama hicho wawahi kule ambapo waliambiwa mbunge wao atahamia.

 Pia walimpongeza Lowassa kwa kufanikiwa kutatua kero za ardhi kati ya wawekezaji na wananchi wa maeneo ya Mto wa Mbu na Meserani kwa kile alichoeleza kuwa endapo asingefanya haraka kutafutia ufumbuzi ingesababisha wananchi wengi kukikimbia chama hicho tawala.

 “Kama wananchi wakiona hawawezi kupata haki ndani ya chama chao (CCM) watatafuta mahali pengine kwa kuipata nje ya chama chao hivyo tunamshukuru Lowassa kwa kuamua kuishughulikia migogoro hiyo ya ardhi na ufumbuzi alioupatia jambo lililosababisha wananchi kutulia” alisema kalanga.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia