WAKAZI wa Tarafa ya Bassotu Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara wametakiwa wasiendeshe shughuli za kilimo na ufugaji kwenye ziwa Bassotu kwani husababisha kina chake kupungua hivyo kuliathiri eneo hilo.
Kutokana na hali hiyo mvua zinaponyesha husababisha udongo huo kuingia ziwani na kupunguza kina cha maji huku jamii inayozunguka eneo hilo kudhani kuwa mabadiliko hayo yanasababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa asasi ya Cedesota,Jackson Muro kwenye mdahalo wa mabadiliko ya tabia nchi na namna ya kupunguza athari zake ulioandaliwa na Mtandao wa asasi za kijamii mkoani Manyara (Macsnet) na The Foundation for Civil Society na kufanyika Bassotu.
Muro alisema udongo huo mlaini unapoingia katika ziwa Bassotu hutengeneza tabaka lenye huziba vishimo vidogo vidogo vilivyopo chini ya ziwa hilo ambavyo vinavyonya maji na kupeleka ziwani.
Aliwataka wakazi wanaozunguka ziwa hilo kutoendesha shughuli za kibinadamu pembezoni mwa ziwa hilo ili kutoendeleza athari hizo na kutosingizia kuwa ni matatizo ambayo yamesababishwa na mabadiliko ya tabia nchini.
Naye,Ofisa Ardhi na Maliasili wa halmashauri ya wilaya ya Hanang’ Kianga Mdundo alisema sheria ndogo ya ziwa Bassotu inawataka wakazi wa eneo hilo kutofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 200 za ziwa hilo.
“Sheria hii mlijiamulia wenyewe na watekelezaji wa kwanza wa sheria hiyo mnatakiwa muwe ninyi wenyewe siyo Mkurugenzi wa wilaya kwani watu wa Bassotu ndiyo mpo ziwani hivyo mtunze mazingira yenu,” alisema Mdundo.
Hata hivyo,Diwani wa kata ya Bassotu,Samwel Qawoga aliwataka wakazi wa vijiji vya Bassotu ambao wananufaika na ziwa hilo kuchukua changamoto zilizopo ili kuhakikisha wanalitunza ziwa hilo.
Qawoga alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuwa ni suala la kitaifa na kimataifa,wakazi wa eneo hilo wanapaswa kusimama kidete katika kuhakikisha kwamba wanayatunza mazingira yanayowazunguka.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia