VIKOBA ARUSHA YAMILIKI BILIONI 7.5

  Maafisa kutoka Mfuko wa Taifa wa  bima ya Afya  (NHIF)wakifuatilia kwa makini Kongamano la Vikoba lililofanyika katika ukumbi wa Olasiti garden na kudhaminiwa Mfukohuo.Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni "Vikoba Chachu ya Maendeleo ya Kweli"


Sehemu ya umati wa wanachama wa VIKOBA mkoa wa Arusha wakifuatilia kwa makini Kongamano la Vikoba lililofanyika katika ukumbi wa Olasiti garden na kudhaminiwa Mfuko wa Taifa wa  bima ya Afya  (NHIF).Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni "Vikoba Chachu ya Maendeleo ya Kweli


Vikundi vya Kuweka akiba na kukopa jijini Arusha maarufu kama VIKOBA wameweza kumiliki kiasi cha shilingi bilioni 5.7 ambazo ni mtaji unaowawezesha kuwakopesha Wanachama wake ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Mwenyekiti wa VIKOBA  mkoa wa Arusha Evance Chipini amesema kuwa vikundi hivyo vinatoa mikopo rahisi ambayo inawasaidia watu kujiendeleza kibiashara ama kuanzisha miradi itakayowakomboa kiuchumi.

Evance Akizungumza katika Kongamano la miaka 10 ya VIKOBA mkoa wa Arusha tangu ilivyoanzishwa mwaka 2005  lililoshirikisha wanachama wote wa vikoba mkoani hapa pamoja na taasisi za fedha amesema kuwa kwa sasa wana vikundi 250 ambavyo vinakadiriwa kumiliki kiasi cha shilingi milioni 35 kila kimoja hadi kufikia jumla ya shilingi bilioni 5.7 hivyo ameiomba serikali ivitambue vikundi hivyo pamoja na kuvisajili ili viweze kutambulika na taasisi za fedha.

“Licha ya mafanikio haya changamoto kubwa tunayokutana nayo hapa ni kupigwa dana dana juu ya usajili wa vikundi vyetu serikalini  wanatuambia twende kwa BRELA ile hali sisi hatuna biashara ya pamoja inayotupa faida tunapaswa kusajiliwa chini ya Idara ya Maendeleo ya jamii,tunaiomba serikali itusaidie katika hili” Alisema Evance

Katibu  Tawala Msaidizi ,huduma za kiuchumi na uzalishaji mkoani Arusha Hargeney Reginald amewaasa wanachama wa VIKOBA kuhakikisha kuwa wanaelekeza mikopo katika vipaumbele walivyojiwekea na kuepuka matumizi mabaya ya fedha ili waweze kuboresha maisha yao na kurejesha mikopo hiyo.

Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Arusha Blandina Nkini amesema kuwa kwa sasa kuna mkakati wa Wizara ya Maendeleo ya jamii kufanya kazi kwa pamoja na Vikundi hivyo vya Wajasiriamali ambavyo asilimia 78% ni kina mama na pia kuwawezesha kupata mikopo ya kuwawezesha Wanawake na Vijana asilimia 10% inayotengwa kila mwaka katika  Halmashauri.

Naye Afisa Utekelezaji Bima ya Afya  kutoka Mfuko wa Taifa wa  bima ya Afya  (NHIF) Desderius Buhiye amewaasa Wanavikoba wajiunge bima ya afya kwani afya njema ni mtaji wa kwanza unaowasaidia Wajasiriamli kufanya kazi kwa ufanisi  na hata wanapokopa inakua rahisi kurejesha.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post