Naibu Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),Dkt Daniel Mushi akiongea na uongozi na wafanyakazi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama cha Eliya Food Overseas Ltd kilichopo wilayani Longido mkoani mkoani Arusha alivyofanya ziara ya kikazi jana akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo
Na Woinde Shizza, LONGIDO
Serikali imeuagiza uongozi wa wilaya ya Longido mkoani Arusha kuhakikisha unadhibiti vitendo vya utoroshaji wa mifugo kwenda nchini Kenya vilivyokithiri na kuathiri uzalishaji katika kiwanda kikubwa cha kuchakata nyama cha Eliya Food Overseas Ltd kilichopo wilayani humo, kiasi kwamba uongozi wa kiwanda hicho umetishia kupunguza wafanyakazi kwa asilimia 50.
Akiongea kiwandani hapo jana, katika ziara yake akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo na bodi ya Nyama ,Naibu Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo),Dkt Daniel Mushi aliutaka uongozi huo unakomesha mara moja vitendo vya utoroshaji wa mifugo kwa kuimarisha vikosi vya doria.
Awali kabla ya kufika katika kiwanda hicho kilichojengwa eneo la mauzo ya nje (EPZ) kwa thamani ya sh, bilioni 17 na kuzinduliwa na rais Samia Suluhu oktoba 18,2021
Naibu katibu mkuu alizungumza na wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Ng'ombe wa Meserani na baadhi yao walikiri kupeleka mifugo nchini Kenya kwa njia za panya wakidai ni hatua ya wao kufuata soko zuri tofauti na wanalopata hapa nchini,hata hivyo walimhakilishia kuwa iwapo kiwanda hicho kitapandisha bei ya kununua mfugo kwa kilo watapeleka kuuza mifugo yao kiwandani hapo.
Dk Mushi aliwataka wafanyabiashara hao kuacha kutorosha mifugo nje ya nchi na kuwaeleza athari za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kilikosesha taifa mapato,kukosa ajira pamoja na kukosa fedha za kigeni kupitia uuzaji wa nyama nje ya nchi unaofanya na mwekezaji wa kiwanda hicho cha Elia Food.
Alisema mwekezaji wa kiwanda hicho amekuwa akilalamika kukosekana kwa mifugo ya nyama wanaoletwa kiwandani katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili kutoka mbuzi na Kondoo 4000 hadi kufikia mbuzi na kondoo 500 kwa siku na hii ni kutokana na mifugo mingi kupelekwa nchi jirani ya Kenya.
"Sisi kama serikali tunaowajibu wa kumlinda mwekezaji kwa nguvu zote kuhakikisha mifugo isitoroshwe na hapa niagize uongozi wa wilaya kupitia mkurugenzi awezeshe kikosi cha kuzuia utoroshaji wa mifugo (SPU)kiweze kufanya doria mara kwa mara na kwa ufanisi mkubwa"
Aidha Naibu katibu mkuu aliutaka uongozi wa wilaya hiyo kuwatumia viongozi wa kimila ,Laigwanani kuwaeleze athari zinazotokana na utoroshaji wa mifugo na kusababisha ukosefu wa ajira , fedha za kigeni na kukosa mapato ya serikali.
Akizungumzia suala la ukame aliutaka uongozi wa wilaya pamoja na mwekezaji kubuni njia mbadala ya chanzo cha maji ili wafugaji waache kuhamisha mifugo yao.
Awali mwekezaji wa kiwanda hicho,Irfhan Virjee alieleza kuwa wakati wanafungua kiwanda hicho mwaka 2019 walikuwa wakizalisha wastani wa mbuzi na Kondoo 300 kwa siku na baadaye walipandisha uzalishaji hadih tani 40 kwa siku sawa na wastani wa mbuzi na kondoo 4000 kwa siku.
Alisema hadi kufikia mwezi juni mwaka huu uzalishaji uliongezeka na kufikia tani 50 kwa siku,lakini baada ya hapo uzalishaji ulishuka kwa kasi kutoka mifugo 4000 kwa siku na kufikia mifugo 500 jambo ambalo limetokana na uhaba wa mifugo .
Alisema kiwanda kimekuwa kikiwalipa vizuri wauzaji wa mifugo ila changamoto kubwa, wafanyabiashara hao wanahitaji kulipwa fedha thasilim bila kupitia mfumo wa benki na hivyo kukwepa Kodi ya serikali kama ambayo wanafanya Nchini Kenya.
"Wakati tunapata changamoto ya mifugo tulifanya uchunguzi na kugundua mifugo mingi inapelekwa nchini Kenya kwa njia za panya ,na hivi sasa tunalazimika kufanyakazi siku tatu kwa wiki na hili tatizo ni zaidi ya miezi miwili sasa "
Aliongeza kuwa tatizo hilo limepunguza pia wastani wa mauzo kutoka dola za kimarekani milioni 3 kwa mwezi na kufikia wastani wa dola milioni 1 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho,Shabir Virjee alipongeza uamuzi wa serikali kuingia ubia wa uwekezaji wa bandari kupitia kampuni ya kigeni ya DP World ya nchini Dubai akidai utakuwa msaada mkubwa kwao kwa kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
"Kwa sisi wafanyabiashara tunaona ujio wa DP World utatusaidia kumaliza tatizo kubwa katika bandari ya Dar es Salaam kwani kwa sasa tunalazimika kutumia bandari ya Mombasa kutokana na ucheleweshaji wa mizigo"
Tags
habari matukio