AI KUFUNGUA FURSA MPYA ZA MAENDELEO AFRIKA
Na Woinde Shizza Arusha
Mkutano wa kimataifa wa teknolojia ya akili bandia (AI) unaofanyika jijini Arusha umeendelea kuvuta wataalam wa TEHAMA, washiriki wa serikali na taasisi mbalimbali za umma, wote wakijadili namna AI inavyoweza kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.
Mtaalam wa TEHAMA, Eliya Kinshaga, amesema AI sasa imekuwa injini kuu ya mageuzi ya kimataifa, hivyo mataifa ya Afrika hayana budi kujenga mazingira wezeshi, kutunga sera madhubuti na kutoa mafunzo kwa wataalamu ili kunufaika kikamilifu na teknolojia hiyo.
Amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya AI yana uwezo wa kupunguza gharama za huduma, kuongeza ufanisi na kuimarisha usalama wa mifumo ya serikali na sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Takwimu wa Benki Kuu ya Uganda, Nalukwago Milly, amesema nchi yake imeanza kushuhudia matokeo chanya ya AI katika usimamizi wa rekodi, ufuatiliaji wa miamala na kufanya maamuzi ya kiuchumi kwa usahihi zaidi.
Amesema mafanikio hayo ni uthibitisho kuwa taasisi za kifedha zinaweza kuboreshwa endapo AI itatumika kwa misingi imara.
Naye Haron Kertish kutoka Wizara ya Kilimo Kenya amesema AI imeleta mabadiliko makubwa kwa kurahisisha usajili wa wakulima, utoaji wa mbolea na uchambuzi wa takwimu za uzalishaji, hatua iliyoinua ufanisi katika sekta hiyo muhimu.
Wadau wa mkutano huo wamesisitiza kuwa Afrika ina uwezo wa kuongoza mageuzi ya AI iwapo serikali na sekta binafsi zitawekeza katika ubunifu, utafiti na ushirikiano wa kikanda kwa maslahi ya uchumi wa bara zima.
Akifunga mjadala huo, mwanzilishi wa Scan Code, Faustin Mgimba, amesema bara hili linapaswa kuongeza uwekezaji kwenye teknolojia zinazobuniwa ndani ili kupunguza utegemezi wa mifumo ya nje.
Amesema ubunifu wa ndani tayari unaonyesha matokeo chanya, na kwamba sera bora na ushirikiano wa sekta zote ni nguzo muhimu katika kujenga mfumo imara wa AI unaokidhi mahitaji ya Afrika.





0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia