NABII MKUU DR. GEORDAVIE ATEULIWA KUWA BALOZI WA UN-PAF AFRIKA MASHARIKI



Na Woinde Shizza 

Nabii Mkuu Mheshimiwa Dr. GeorDavie K. Moses, Kiongozi wa Kanisa la Ngurumo ya Upako lililopo jijini Arusha, ameteuliwa rasmi kuwa Balozi na Mwakilishi wa Shirika la Mabalozi wa Amani la Umoja wa Mataifa (UN-PAF) kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Uteuzi huo ulifanyika jijini New York, nchini Marekani, tarehe 9 Septemba 2025, na kutangazwa rasmi na Mwenyekiti wa Dunia wa UN-PAF, Mhe. Balozi Kingsley Ossai, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa shirika hilo linalosimamia masuala ya amani duniani.



Mara baada ya uteuzi huo, Balozi Ossai alituma barua za utambulisho rasmi kwa Serikali ya Tanzania, Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, pamoja na Ubalozi wa Marekani, kwa lengo la kumtambulisha Mhe. Dr. GeorDavie katika nafasi yake mpya ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka makao makuu ya UN-PAF, uteuzi wa Dr. GeorDavie umetokana na mchango wake mkubwa katika kuhubiri amani, mshikamano na maendeleo ya kijamii, sambamba na jitihada zake za kusaidia makundi mbalimbali ya kijamii kupitia miradi ya kiuchumi na kielimu.

Mhe. Dr. GeorDavie, ambaye pia ni Mlezi wa Jumuiya ya Maaskofu na Manabii Tanzania (JMAT), amekuwa akijulikana kwa juhudi zake katika kueneza ujumbe wa upendo na kusaidia vijana pamoja na wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia programu za ujasiriamali.

Aidha, Dr. GeorDavie amekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za dini, serikali na jamii kwa ujumla, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kama msingi wa maendeleo endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa uteuzi huu, Tanzania imepata heshima nyingine kimataifa, kwani hii ni mara chache kwa kiongozi wa kiroho kutoka nchini kuteuliwa kushika nafasi ya kibalozi ndani ya shirika linalohusiana moja kwa moja na Umoja wa Mataifa.



Shirika la UN-PAF limeeleza imani kubwa kuwa chini ya uwakilishi wa Mhe. Dr. GeorDavie, Afrika Mashariki itanufaika na fursa zaidi za diplomasia ya amani, ushirikiano wa kimataifa na miradi ya maendeleo inayolenga kuinua ustawi wa wananchi.

Akizungumza mara baada ya uteuzi huo, Mhe. Dr. GeorDavie alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa heshima hii kubwa. Nitaitumia nafasi hii kuimarisha umoja, amani na upendo si tu kwa Afrika Mashariki, bali pia kwa dunia nzima. Ni wajibu wetu kama viongozi kuhakikisha tunakuwa daraja la matumaini kwa jamii zetu.”

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia