Juni 12, 1964, Nelson Mandela alihukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya hujuma dhidi ya Serikali ya kibaguzi ya Makaburu.
Hata hivyo Mandela alitumikia kifungo hicho kwa
miaka 27 na kutoka akiwa mtu aliyebadilika kitabia, akiwa mtulivu, akiwa
na hekima, mwenye busara na mwenye kuheshimika katika jamii.
Mandela alianza kutumikia kifungo katika jela
iliyopo kwenye kisiwa cha Robben kilichopo kwenye bahari ya Atlantic
umbali wa kilometa 12 kutoka mji wa Cape Town, alimotumikia kifungo kwa
miaka 18, na mwaka 1982 aliondolewa ndani ya kisiwa hicho na kuhamishiwa
kwenye gereza pia lenye ulinzi mkali la Pollsmoor lililopo Cape Town na
siku chache kabla ya kuachiwa huru alihamishiwa gereza lililopo mjini
Cape Town la Victor Verster.
Kisiwa cha Robben kwa takriban miaka 400 iliyopita
kimekuwa kikitumika kama eneo la kuadhibu watu, kuweka watu katika
maisha ya kuwatenga na kuwafunga jela. Ni kisiwa kwa ajili ya watu
wasumbufu wa kisiasa, wasumbufu katika jamii na watu wasiotakiwa katika
jamii.
Kama ilivyo kwa viongozi na wanaharakati wengine
wa ukombozi wa kiafrika waliopata changamoto za Serikali za kikoloni kwa
kukamatwa, ambao baadaye walikuja kushika uongozi wa nchi zao, kama
vile Kwame Nkrumah wa Ghana, Jomo Kenyatta wa Kenya na Robert Mugabe wa
Zimbabwe, Mandela naye alipotoka jela alikuwa Rais wa kwanza mweusi
nchini Afrika Kusini.
Gereza la Kisiwa cha Robben, lililofahamika kwa
jina la gereza ndani ya gereza, lilikuwa ni gereza lenye zahama na
ukiwa. Kufungwa ndani ya gereza hilo maana yake ni muda mwingi kufanya
kazi za suluba, lakini kulikuwa na fursa kwa mfungwa kupata muda wa
kujisomea, kufanya mijadala na kujipima. Miongoni mwa masharti ya
kushikilia maadili ndani ya gereza hilo ni kwa wafungwa kujikita kwenye
kusoma na kufanya mijadala. Tabia ya Mandela na uongozi wenye weledi ni
matokeo ya maisha ya jela au ‘Chuo Kikuu cha Kisiwa cha Robben.’
“Hakuna zaidi ya kuelekeza akili zako kwa kuwa
mtulivu zaidi kwa kukubali ukweli wa jamii yako,” alisema Mandela.
Mwanzoni mwa mwaka 1972, alipewa ofa ya kutoka jela kwa sharti la
kutangaza kukomesha vurugu dhidi ya Serikali ya Makaburu, ofa mabayo
aliikataa akisema kuwa Serikali ndiyo imekifanya chama cha ANC kutumia
njia ya uanaharakati.
Maisha ya jela ndiyo yaliyombadili Mandela na kuwa
kiongozi mwenye ushawishi, ambapo akiwa gerezani alijifunza kuhusu
hisia za binadamu na namna ya kuondoa hofu na mambo yasiyo ya usalama
kwa wengine. Akiwa gerezani Mandela aliwavutia askari magereza kwa namna
alivyokuwa mtetezi wa haki, mweye heshima na mwenye uelewa wa masuala
ya kisheria, ambapo ndani ya gereza la Kisiwa cha Robben alikuwa
kiongozi wa wafungwa wenzake.
Kwa mujibu wa taarifa askari magereza walikuwa chini ya uongozi wa wafungwa na wafungwa walikuwa chini ya uongozi wa Mandela.
Mwandishi wa habari Eddie Koch aliandika kwenye
magazeti ya Mail na Guardian kuwa selo namba saba alimokuwa akiishi
Mandela, lilikuwa eneo lenye harakati nyingi za ulinzi mkali ndani ya
gereza hilo kwa kila Jumamosi ya wiki.
Wakati Mandela akiwa ndani ya gereza hilo kulikuwa
na mikwaruzano ya wafungwa, kutoka kitengo cha kijeshi cha ANC, chama
cha Pan Africanist Congress na wanaharakati wa Steve Biko’s Black.
Vurugu ndani ya gereza hilo zilifanyika kwa misingi ya kupingana watu
binafsi na tofauti ya itikadi, ambapo vurugu hizo zilikuwa kipimo cha
mbinu za uongozi wa kidiplomasia wa Mandela na wenzake.
Taarifa zilisema wafungwa wengi wapya walipelekwa
kwenye gereza hilo la Kisiwa cha Robben, kama vile viongozi wa wanafunzi
wa Soweto, wawakilishi wa baraza waliochochea vijana hadi wakaazisha
vurugu nchini humo mwaka 1976, hawakuwa na ufahamu kuhusu hali ya
kisiasa ndani ya gereza hilo.
Hivyo ilikuwa ni jukumu la Mandela na wenzake kuwaelimisha na
kuwapa taratibu za gereza hilo wafungwa hao wapya vijana, gereza hilo
lilikuwa sehemu huru kwa wasomi kutumia vipaji vyao. Gereza la Kisiwa la
Robben lilijengwa kwa namna ambayo limezuia mawasiliano kati ya
uongozi, askari au viongozi waandamizi wa harakati.
Wafungwa ambao ni viongozi waandamizi katika vyama
vyao nje ya gereza, kila mmoja alifungwa kwenye selo yake iliyokuwa
kwenye jengo B. Wahalifu sugu na wapiganaji wa msituni ambao lengo lao
ni kuuondoa utawala wa makaburu waliwekwa kwenye jengo A ambalo
limetengwa na majengo mengine.
Jengo G limejengwa kwa wafungwa wengi kuishi
katika selo moja. Siku za nyuma wafungwa wenye asili ya Kihindi walikuwa
wakitenganishwa na wafungwa wenye asili ya waafrika weusi.
Mandela siku zote alipopata fursa ya kuzungumza na
askari magereza wa Afrikaner aliwataka kujielekeza kwenye mstari wa
fikira za ANC. Hali hiyo ilimsaidia kujiimarisha kwa kuwa na mbinu mpya
kila mara za kujenga hoja.
Hata hivyo, rafiki wa Mandela, Walter Sisuli
ambaye walikuwa naye gerezani, alichukulia mazungumzo hayo kama mwanzo
wa makubaliano na serikali ya kibaguzi.
Mandela pia akiwa gerezani alitumia muda huo
kujiendeleza katika elimu ya sheria. Alibaini kuwa elimu hiyo inamsaidia
kuweka msingi kwa makubaliano ya mwisho yasiyo ya kumwaga damu, kwa
mslahi ya Afrika Kusini ijayo.
Insha na maandiko ambayo hayakuchapishwa
aliyoyaandika akiwa gerezani yaliifanya Afrika Kusini iwe kama
mshangiliaji, ilionyesha usomi zaidi na uasilia kuliko ule wa awali
wakati wa mapambano na wakoloni. Alikuwa na matarajio ya kupata ukweli.
Mandela aliona jela kama vile maabara ya namna
rangi tofauti zinaweza kuelewana na kuishi kwa utulivu. Aliona gereza
kama mwakilishi wa jamii wa maelewano nchini Afrika Kusini ambayo
yanaweza kudumishwa.
Hata hivyo, mkuu wa gereza Colonel Willie mwaka
1971 alizungumzia uwezo na utayari wa Mandela wa kuongoza serikali ya
mpito nchini Afrika Kusini: “Mandela ana kariba ya kipekee. Amepata
uzoefu wa mabadiliko ya kisiasa. Sidhani kama anasubiri kwa ajili ya
kulipa kisasi. Sijaona chuki kwa yeyote miongoni mwao, lakini Mandela
ana nafasi kubwa ya kuwashawishi.”
Alisema akiwa gerezani amekuwa akishirikiana na
wazungu na wahindi ambapo walimuamini kwa asilimia kubwa, kwakuwa hakuwa
anazungumzia kulipa kisasi kwa watu wa rangi nyingine.
Kilichompeleka jela
Mandela ambaye alikuwa kiongozi wa jumuia ya
African National Congress (ANC), ambayo ilikuwa ikipinga ubaguzi wa
rangi, mwaka 1956 alikamatwa kwa tuhuma za uhaini, lakini aliachiwa
huru. Mwaka 1960 ANC ilipigwa marufuku na Serikali ya Makaburu.
Mwaka 1961, Mandela na viongozi wengine wa ANC waliunda jumuia
nyingine iliyoitwa Umkhonto we Sizwe (MK), ambayo ilikuwa ni kitengo cha
kijeshi cha ANC. Desemba 16, 1961, MK, ambayo Mandela alikuwa mkuu wake
wa majeshi, kilifanya shambulio la bomu kwenye maeneo ya Serikali na
walianzisha mapigano ya msituni. Mandela alikamatwa Agosti 5, 1962, na
alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kuchochea wafanyakazi
kugoma katika mgomo wa wafanyakazi uliotokea mwaka 1961.
Julai 1963 serikali ilishambulia shamba la
Lilliesleaf lililokuwa Rivonia, ambalo lilikuwa likitumiwa na ANC kama
maficho yao. Viongozi 19 wa ANC walikamatwa na kukutwa na nyaraka
zilizoonyesha uhusiano wao na MK na mipango ya kufanya mashambulizi
ikiwemo vita vya msituni.
Serikali ya makaburu iliwafungulia mashitaka
viongozi 11 wa ANC, chini ya sheria ya uhalifu wa kufanya hujuma ya
mwaka 1962. Wakati wa kesi Mandela hakutaka kuwa na shahidi na badala
yake alielezea historia ndefu ya malengo ya ANC na MK, ambapo alikiri
baadhi ya makosa lakini alijitetea kwa kosa la kutumia vurugu kudai
haki. Na Julai 1964 alihukumiwa kifungo cha maisha jela. (NMG).