Mamlaka
ya Hifadhi za Taifa TANAPA imezindua tuzo za umahiri wa habari kwa Mwaka 2013
na kuwataka Wanahabari kote nchini kujitokeza katika kinyang’anyiro hicho
kinachozipambanisha kazi bora za habari zinazoyaangalia maeneo ya uhifadhi hapa
nchini na utalii wa ndani.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari jijini Arusha, Meneja Uhusiano wa TAPANA Pascal
Shelutete amesema kuwa lengo la tuzo hizo ni kuendelea kuwahamasisha Waandishi
wa Habari kuona wajibu wao wa kitaaluma katika kuibua taarifa mbalimbali zenye
usahihi juu ya changamoto na mafanikio yanayoizunguka sekta ya utalii hapa
nchini.
Shelutete
amesema tuzo hizo zinafanyika wakati ambapo sekta ya Utalii hapa nchini imekuwa
ikikabiliwa na vitendo vingi vya ujangiri vinavyotia dosari harakati za
uhifadhi wa maliasili huku katika suala la Utalii wa ndani bado Watanzania
hawajitokezi kwa wingi kuzitembelea Hifadhi za Taifa.
Katika
tuzo za Mwaka huu TANAPA imefanya maboresho ya zawadi hususani katika viwango
vya fedha ambapo Washindi wa kwanza kwa kila kipengele watakabidhiwa Shilingi
Milioni mbili, washindi wa pili Shilingi milioni moja na nusu na washindi wa
tatu shilingi milioni moja huku baadhi ya washindi hao wakipata nafasi ya
kujifunza uhifadhi na utalii wa ndani katika hifadhi za Tanzania na nje ya
nchi.
Mwaka
2012 katika tuzo za umahiri wa habari za uhifadhi na utalii wa ndani
Wafanyakazi wawili wa Kampuni ya Sahara Media Group SMGL walipata tuzo kwa
upande wa Televisheni na Magazeti kupitia habari na vipindi walivyoviwasilisha
katika tuzo hizo zinazoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa TANAPA.