MTOTO WA KIGOGO MKOANI ARUSHA AMPIGA MFANYAKAZI WA BAR RISASI

 
Jeshi la polisi mkoani Arusha limemshikilia na kisha kumwachia “chapchap” mtoto  wa mwenyekiti wa CCM wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro na mfanyabiashara maarufu nchini,Oscar Themi  kwa kosa  la kumpiga risasi ya kichwa mhudumu wa bar ya Empire iliyopo eneo la Shoprite jijini Arusha.

Mtuhumiwa huyo ,Dereck Themi  alishikiliwa na polisi mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya kutofautiana na mhudumu huyo wakati alipompatia bili ya vinywaji aliyokuwa akitumia ndani ya bar hiyo kabla ya kumtandika risasi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa mnamo novemba 29 mwaka huu majira ya saa 7.30 usiku mtoto huyo wa kigogo alimfyatulia risasi mhudumu huyo aliyetambulika kwa jina la Witness Erasto wakati alipompatia bili ya vinywaji.

Mashuhuda walidai kuwa kulitokea na hali ya tofauti kati yao ambapo  Themi alikubali kulipa bili hiyo ambapo alichukua fedha na kisha kumwekea katika matiti yake na ghafla kuchomoa bastola yake na kisha kumtandika eneo la kichwa.

 Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa mara baada ya tukio hilo ndipo mtuhumiwa alijaribu kukimbia nje ya bar hiyo kuelekea usawa wa eneo la maegesho la magari lakini kabla hajafika alifyatua risasi nyingine zaidi ya tano hali iliyopelekea tafrani katika eneo la Shoprite.

Hatahivyo,taarifa hizo zimedai kuwa askari mmoja aliyekuwa akilinda benki ya Exim iliyopo ndani ya eneo hilo la Shoprite alimvizia kimafia na kisha kumnyang”anya bastola hiyo mtuhumiwa kabla ya kuwataarifu polisi waliofika eneo hilo na kisha kumfikisha katika kituo kikuu cha polisi cha kati.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa katika kituo hicho na kisha kukabidhi bastoa hiyo pamoja na maganda matano ya risasi ambapo baada ya muda aliwasili mdogo wake aliyetambulika kwa jina la Bernad Themi aliyechukua mali zake na fedha.

Akihojiwa na gazeti hili majeruhi wa tukio hilo Erasto alisema kuwa hawezi kuongea chochote kwa kuwa hali yake ni sio nzuri lakini alipotafutwa mmiliki wa bar hiyo,Tumaini Ulomi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa tayari wameshafungua mashtaka mbalimbali ikiwemo hasara aliyoipata siku ya tukio.

Mmiliki huyo alisema kuwa mara baada ya milio ya risasi kuanza kurindima ndani ya bar yake wateja mbalimbali wakiwemo watalii walitokomea kusikojulikana bila kulipa hali ambayo imemtia hasara kubwa.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa kifupi kwamba bado wanafanya uchunguzi wa kina kabla ya kulifikisha suala hilo mahakamani.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post