Mombasa. Ushujaa wa kipa namba moja wa Kilimanjaro Stars, Ivo Mapunda umeivua ubingwa Uganda na kuiingiza Stars nusu fainali ya Kombe la Chalenji.
Stars itacheza na Kenya iliyoilaza Rwanda bao 1-0
katika mechi nyingine ya robo fainali iliyochezwa jana jioni kwenye
Uwanja huohuo wa Manispaa unaobeba mashabiki 15000.
Uganda iliutwaa ubingwa huo mwaka jana mjini
Kampala ikiwa haijafungwa bao hata moja kwenye mechi zake zote, Uganda
ilikuwa inaelekea kutimiza rekodi hiyo lakini jana Stars ikatibua mambo.
Awali kwenye mechi za makundi Uganda ilikuwa haijaruhusu bao lolote.
Mapunda anayeichezea Gor Mahia ya Kenya alipangua
penalti mbili za Uganda ambayo kocha wake, Sredejovic Milutin ‘Micho’
alijitetea kwamba penalti hazina ufundi na wala Stars haijafanya cha
ajabu. “Hakuna cha ajabu kwenye penalti, hakuna fundi.”
Licha mwamuzi Msomali, Wish Wabarow kuonekana
kuzidiwa na mchezo, mechi hiyo ilimalizika kipindi cha kwanza Stars
ikiongoza mabao 2-1 huku ikishangiliwa na uwanja mzima uliokuwa
umetawaliwa na Wakenya na Watanzania walioingia kupitia Lungalunga,
Tanga.
Straika wa Uganda anayewindwa na Yanga, Danny
Serunkuma ndiye aliyefunga bao la kwanza dakika ya 16 akipiga shuti kali
katikati ya mabeki wa Stars lakini dakika mbili baadaye Mrisho Ngassa
alisawazisha kwa shuti kali kutoka nje kidogo ya boksi likamshinda kipa
Benjamin Ochan.
Ngassa huyohuyo akapiga bao la pili kwenye eneo
lilelile dakika ya 38. Mchezo huo uligubikwa na aibu ya aina yake
kutokana na kutokuwepo kwa wasaidizi wa Msalaba Mwekundu kwa kile
kilichodaiwa kwamba hawajalipwa chao na Cecafa.
Timu hizo zilishambuliana kwa kasi kipindi cha
kwanza ambapo mastraika Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu waliipa shida
Uganda ambayo kwa siku ya jana straika wake, Danny Serunkuma ndiye
aliyeisumbua zaidi Stars.
Kipindi cha pili dakika 52 Aboubakar Salum ‘Sure
boy’ ambaye alikuwa akichezesha timu, alionyeshwa kadi nyekundu baada ya
kumkanyaga beki wa kushoto wa Uganda, Godfrey Walusimbi.
Dakika ya 75 beki mrefu wa Uganda alifunga bao laini baada ya Ivo kuutema mpira wa kona ya Wakiro Wadada.
Baada ya kumalizika kwa dakika 90, zilipigwa
penalti ambapo Uganda ilikosa tatu na Stars ikakosa mbili. Penalti za
Stars zilipigwa na Erasto Nyoni na Mbwana Samatta (walikosa), Amri
Kiemba, Athuman Idd na Kelvin Yondani. Uganda walipiga Danny Walusimbi
(alikosa), Emanuel Okwi, Aucho Khalid (alikosa), Hamis Kiiza na
Serunkuma aliyekosa penati ya mwisho na kuivusha Stars.
Ivo Mapunda ambaye alikuwa akishangiliwa na
mashabiki wengi wa Kenya alisema: “Siamini kwamba tumeshinda, ni Mungu
tu. Mpira ulikuwa mgumu sana na tulicheza na timu ngumu ambayo tumeitoa
kwa juhudi binafsi za wachezaji.”
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia