India, Ufaransa, Marekani, Canada zaomboleza kipekee

 
Wakati Bara la Afrika likiendelea na maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini na mkombozi aliyepinga siasa za ubaguzi za makaburu, Nelson Mandela, mataifa mengine duniani yameonyesha kufanya maombelezo katika namna mbalimbali.
Pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mandela na wananchi wa Afrika Kusini, viongozi wa mataifa makubwa duniani wameonyesha kuguswa na msiba huo kiasi cha kuomboleza kwa namna tofauti tofauti.
India
Hii inaweza kuwa ni nchi mojawapo ambayo imetangaza siku nyingi zaidi za maombolezo kwa ajili ya kifo cha Nelson Mandela kutoka nje ya Bara la Afrika.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha Mandela, Serikali ya India kupitia Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Manmohan Singh aliwatangazia siku tano za maombelezo na kuamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti katika kipindi hicho cha maombolezo.
Sambamba na hilo, Singh  alimwelezea  namna kiongozi huyo wa Afrika alivyokuwa shujaa katika kupinga mfumo wa kibaguzi.
Ufaransa
Kuonyesha kuwa taifa hili pia limeguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huu, jengo refu zaidi mjini Paris la Eiffel Tower liliwashwa taa zenye rangi zilizopo kwenye Bendera ya Afrika Kusini.
Picha zilizopigwa katika jengo hilo mpaka siku ya jana, linaionyesha likiwa limenakshiwa na taa zenye rangi tano  za bendera hiyo zikiwemo nyekundu, kijani, nyeusi, njano na nyeupe.
Marekani
Taifa hili lenye nguvu duniani limeonyesha heshima kubwa kwa Nelson Mandela kwa kupeperusha bendera zake nusu mlingoti nchi nzima na kuweka siku tatu za maombolezo.
Kana kwamba hiyo haitoshi taa zenye rangi ya Bendera ya Afrika Kusini zilionekana kung’arisha jengo la Empire state lililopo NewYork na Hoteli ya Omni iliyopo Dallas.
Mjini Washington jengo la Ubalozi wa Afrika Kusini lilitawaliwa na taa hizo pamoja na bendera za nchi hiyo hali iliyosababisha mwonekano wa eneo hilo kubadilika kabisa.
Pia  kiongozi wa taifa hilo Rais Barack Obama alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Graca Machel ambaye ni mjane wa Mandela.
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani ilisema kuwa Obama alimpigia simu mama Machel kwa lengo la kumtumia salama za rambirambi.
Canada
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini Canada, Waziri Mkuu Stephen Harper amewaalika mawaziri wakuu wengine wastaafu wa nchi hiyo kuungana naye kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mazishi ya Nelson Mandela.
Australia na Uingereza
Kama ilivyo kwa nchi nyingine, mataifa haya pia yalitangaza siku za maombolezo sanjari na kupeperusha bendera zake nusu mlingoti kuashiria maombolezo ya kifo cha kiongozi shujaa na mahiri barani Afrika, hayati Nelson Mandela.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post