Wabunge jana waliumbuana kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma huku Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe akituhumiwa kuagiza kubadilishwa kwa tiketi ya ndege ya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Joyce Mukya ili afupishe ziara yake ya kikazi huko Marekani na kwenda Uarabuni kwa shughuli binafsi.
Mbali ya Mbowe, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey
Zambi (CCM) anadaiwa kuchukua posho ya Kamati ya Hesabu za Bunge (PAC),
kwa safari ya kwenda Dubai na wenzake lakini badala yake akaenda Mbeya
kwenye ziara za chama chake.
Malumbano hayo yaliibuka jana baada ya Mbunge wa
Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), kuomba mwongozo wa Spika
akitaka kufahamu kauli ya ofisi yake kwa Mbowe kutumia nafasi yake
kumrudisha mbunge ambaye ameshatumia fedha za Serikali.
Alidai kwamba Mbowe aliagiza Mukya aanze safari
Desemba Mosi, mwaka huu kutoka New York, Marekani ili aende Dubai, Falme
za Kiarabu (UAE) kabla ya kwenda Dar es Salaam, Desemba 3, mwaka huu.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo jana, Mbowe alisema
hawezi kuzungumza chochote kwa kuwa hakuwapo bungeni akisema alikuwa
Dar es Salaam kwenye kikao.... “Siwezi kusema lolote mpaka nipate
hansard (kumbukumbu rasmi ya Bunge) na kutoka kwa wabunge wangu walioko
Dodoma kujua nini kimesemwa.”
Akiomba mwongozo Nchemba ambaye pia ni Naibu
Katibu Mkuu wa CCM alisema: “Jambo hili limechukua taswira kama ni Bunge
lote linafanya mambo haya na limevunja heshima ya Bunge. Jambo hili
linatuvunjia heshima hata watu ambao tuna maadili ya uongozi na
tunaliheshimu taifa letu...
“Pamoja na kuwa jambo hilo lilikuwa la binafsi,
lakini kuna ujumbe tumeupata kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani amemzuia
mbunge wake kusafiri na magazeti yakaandika kwamba wana mahusiano. Mimi
sipendi kwenda kwenye uhusiano, nataka kwenye taswira ya Bunge na
Taifa.”
Alisema Bunge linapopanga safari za wabunge linazingatia wa chama tawala na wapinzani ili kuweka uwakilishi.
Nchemba alisema Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Chadema, aliandika ujumbe mfupi wa simu kwa mtumishi mmoja wa Bunge
akitaka kubadilishwa kwa tiketi ya ndege ya mbunge.
Aliusoma ujumbe huo: “Rejea mazungumzo yetu bwana
Kabunju kuhusu mheshimiwa Joyce Mukya ambaye yupo safarini. Nitashukuru
kama utambadilishia booking (safari) yake ili aweze kurudi, aondoke New
York tarehe moja Desemba na kurejea Dubai baadaye ataunganisha kurejea
Dar es Salaam by Mbowe kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni nakala kwa
Joyce Mukya.” Kabunju S. Kabunju ni Ofisa wa Bunge anayeshughulikia
masuala ya usafiri.
Nchemba alisema: “Ameshakatiwa tiketi, ameziba
nafasi ya kwenda kuliwakilisha taifa kule, anamwita arudi Dubai na ni
mbunge viti maalumu. Je, hili lina taswira gani kwa taifa na kiti chako
kinatoa kauli gani kwa watu ambao wanakwenda kutumia fedha za Serikali
kwa mambo binafsi, Dubai?” alisema.
Pia alitaka kufahamu Bunge linachukua hatua gani
stahiki kwa mbunge anapoingilia kazi za kiti na pia watumishi
wanapoingiliwa na kubadilisha yale waliyotumwa kwa ajili ya Serikali.
Tuhuma za Zambi
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde
alisema Nchemba anaegemea zaidi wabunge wa upinzani wakati wapo wa CCM
waliochukua posho.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, yaliyosemwa na magazeti na
mwombaji wa mwisho (Nchemba), alipokuwa anatoa mwongozo amejaribu
kuainisha wabunge wa upande mmoja wa upinzani,” alisema.
Alimtaja Zambi kuwa alichukua fedha ili kwenda
Dubai na wenzake lakini badala yake alikwenda Mbeya wakati Katibu Mkuu
wa CCM, Abdulrahman Kinana alipokuwa katika ziara mkoani humo. Zambi pia
ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.
“Tunaomba mwongozo wako namna gani hili suala
litachukuliwa hatua na wala siyo kufanya propaganda za kisiasa ndani ya
Bunge lako,” alisema Silinde.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema kuna mambo mengi yanayofanyika ndani ya Bunge hilo lakini hayasemwi.
“Kuna watu wameandikwa ndani ya magazeti wanaiba
vidani licha ya kutosemwa lakini imeonekanika huku. Mambo ya mapenzi ni
ya mtu na mtu wake, humu kila mtu ana mpenzi wake,” alisema.
Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe alisema: “Kamati ya PAC ambayo inahusika na
masuala ya fedha za umma tayari imeshamwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), afanye uchunguzi kuhusiana na safari zote ili
jambo hili liweze kufika mwisho.”
Alisema taarifa hiyo itapelekwa kwa Spika na kama atapendezwa italetwa bungeni ili jambo hilo liweze kumalizika.
Akijibu mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge
aliyekuwa akiongoza shughuli za jana asubuhi, Mussa Azzan Zungu alisema:
“Nimepokea miongozo yote na kiti kinasema hakina lazima ya kujibu sasa
hivi, kitatoa mwongozo baada ya kufikiria na kuyatafakari hapo
kitakapopata nafasi.”
Hata hivyo, kabla ya kuahirisha Bunge jana mchana,
Zungu alisema suala hilo ni la kiutawala na masuala yote yanayohusu
masuala ya fedha yanatawaliwa na sheria na kanuni za fedha.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki iliyopita na
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy alipokuwa akichangia
taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac)