Serikali imeombwa kuanzisha bodi
ya zao la ufuta kama ilivyoanzisha bodi ya mazao ya pamba, kahawa na katani,
ili kuwawezesha kuwanyanyua kiuchumi wakulima wa zao la ufuta ambalo hivi sasa linalimwa
kwa wingi hapa nchini.
Imeelezwa kwamba bodi hiyo ya zao
la ufuta endapo itaanzishwa itawasaidia wakulima wake kunufaika kiuchumi, kwani
watakuwa na soko la uhakika kuliko hivi sasa wanapotapeliwa na walanguzi
wanaonunua zao hilo shambani mwao.
Ombi hilo lilitolewa na
baadhi ya wakulima wa zao la ufuta wa Tarafa ya Mbugwe, Wilaya ya Babati, katika
Mkoa wa Manyara, ambao walijengewa uwezo wa kulima zao hilo na shirika lisilo
la kiserikali la Farm Africa.
Mmoja kati ya wakulima hao
Theresia Njaiko mkazi wa kijiji cha Mwada, alisema endapo Serikali ingeanzisha
bodi ya zao la ufuta wakulima wengi nchini wangefaidika kwenye uuzaji kupitia
zao hilo linalolimwa kwa wingi nchini.
Mkulima mwingine wa ufuta Khadija
Juma mkazi wa kijiji cha Magugu, alisema japokuwa zao hilo halina bodi kama
mazao mengine ila wanategemea shirika la Farm Africa kwa kuwapatia elimu ya
kilimo hicho, mbegu, dawa na masoko.
Tabu Issa wa Magugu aliiomba
Serikali kutupia jicho kwenye zao hilo, kwani hivi sasa wakulima wengi
wamefaidika kupitia ufuta hivyo Serikari iwageukie na wao, japokuwa wanawezeshwa
na shirika hilo lisilo la kiserikali la Farm Africa.
Kwa upande wake, mkulima wa kijiji
cha Mwada Lucas Said alilishukuru shirika la Farm Africa kwa kuwawezesha
mafunzo, kuwapatia mbegu na kuwatafutia soko la ufuta, hivyo kuwasaidia
kuwanyanyua kiuchumi kupitia zao hilo.
Mkulima Juliana Agustino wa Mwada,
alitoa wito kwa Serikali iwasaidie wakulima wa ngazi ya chini, kuwawezesha
kushiriki maonyesho ya kilimo ya nane nane ili waonyeshe mazao yao na pia
kujifunza kupitia wakulima wengine.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia