Mkuu
wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo ametamka ya kwamba
miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimnyima usingizi na hata kumuumiza
kichwa ni pamoja na suala la kukosekana kwa amani na usalama katika
mkoa wa Arusha.
Mulongo,alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita katika
mkutano wa kujadili suala la amani na usalama katika mkoa wa Arusha ambao
uliandaliwa na ofisi ya msajili mkuu wa vyama vya siasa hapa nchini.
Akiongea kwa hisia Mulongo alisema kuwa kiongozi yoyote
anayeongoza mkoa usiokuwa na amani na usalama hata yeye binafsi anakosa amani
moyoni hata kama akijifariji kwa kujifungia ofisini kwake.
“Unapoongoza mkoa
usiokuwa na amani unakosa amani wewe mwenyewe hata kama ukijifungia ofisini
peke yako na kujifariji”alisema Mulongo
Hatahivyo,Mulongo alienda mbali zaidi na kudai ya kuwa
vitendo na mazingira ya kutoaminiana tangu uchaguzi wa mwaka 2010 ndio sababu
kuu iliyochangia vurugu katika baadhi ya maeneo ukiwemo mkoa wa Arusha.
Alisema kuwa mara baada ya uchaguzi huo kumalizika kuna
baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa walijitokeza hadharani na kuikataa serikali
iliyoapishwa madarakani hivyo na kudai dhambi ile ilichangia kutafuna amani ya
nchi hadi sasa.
Mkuu wa mkoa huyo alimshukuru msajili wa vyama vya siasa
nchini,Jaji Francis Mutungi kwa kuumiza kichwa kutafuta suluhu ya amani katika
mkoa wa Arusha huku akihaidi ofisi yake kuhakikisha wanakamilisha maandalizi ya
mkutano wa amani unaotaraji kufanyika desemba 6 mwaka huu jijini hapa.
Mbunge wa jimbo la Arusha mjini,Gobless Lema sanjari na
mbunge wa viti maalumu,Mary Chatanda wote kwa pamoja walisema kuwa suala la
amani katika mkoa wa Arusha limekuwa likiwaumiza vichwa mara kwa mara huku
wakihaidi ushirikiano wa dhati na dola katika kutafuta suluhu ya amani hiyo.
Kwa kauli moja walisema kuwa siasa za ubaguzi na chuki zilichangia
kwa kiasi kikubwa kupoteza amani ya mkoa wa Arusha huku wakidai kuwa watakuwa
kielelezo cha amani kwa wanachama wao katika mkoa wa Arusha.
Katika mkutano huo mojawapo ya maazimio yaliyoafikiwa ni
pamoja na kufanyika kwa mkutano mkubwa wa amani unaotaraji kufanyika desemba 6
mwaka huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambapo vyama vyote vya siasa,waumini
wa dini na wasio na dini sanjari na wakazi wa mji wa Arusha watashiriki kwa
lengo la kuombea amani katika mkoa wa Arusha.