HAWA NDO WASALITI WA MWALIMU NYERERE :WARIOBA ALONGA

MWENYEKITI wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph WariobaMWENYEKITI wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amedokeza kuwa kwa tabia na mwenendo wao, watawala wamemsaliti Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Jaji Warioba amekemea pia tabia ya watawala kumtumia Mwalimu Nyerere kama hirizi wanapotaka kupitisha mambo yao, huku wakimsaliti kwa matendo yao.
Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 cha ITV juzi, Jaji Warioba aliwajibu viongozi wa serikali, wana CCM na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaomshambulia kwamba amemsaliti Mwalimu Nyerere.
Alisisitiza kuwa kamwe hajamsaliti Baba wa Taifa Julius Nyerere kwa kuleta mapendekezo ya serikali tatu, bali tume imetazama mapendekezo na hali halisi ya wakati tuliomo.
Badala yake Jaji Warioba amesema kuhusu kumsaliti Mwalimu kuwa; Mwalimu Nyerere hakuwa na mawazo ya mgando, kwa hiyo wasingemtegea kwamba wakati wote yale aliyokuwa nayo kama angekuwepo angekuwa na hayo hayo.
“Mwalimu alikuwa anafuata wakati ulivyo, lakini kubwa zaidi hao wanaosema hivyo ndio wamemsaliti Mwalimu… Nilisema Mwalimu ametuachia muungano ambao Bunge la Muungano lilikuwa na madaraka kamili, wameharibu… Mahakama ilikuwa na madaraka kamili wameharibu.
“Aliacha nchi moja, wamezigeuza nchi mbili, wakati wa Mwalimu mizinga ilikuwa inapigwa kwa rais wa nchi, sasa hivi wanapiga mizinga kwa marais. Wamevuruga muungano, hawaambiliki wanakimbilia kumgeuza Nyerere kama hirizi,” alisema.
Jaji Warioba alifafanua kuwa wakati wa Mwalimu mambo 22 ya muungano yaliyomo kwenye katiba, alipotoka kama rais yalikuwa 21 na lile la 22 kuhusu vyama vya siasa lilikuja baadaye.
“Lakini hata Rais Kikwete alipokwenda kwenye Bunge la Katiba alieleza kila moja ya mambo yale yaliingiaje kwenye katiba na lini yaliingia. Yaliingia kikatiba, wao wameyaondoa kinyemela bila kupitia katiba.
“Mwalimu alikuwa analinda katiba, sasa wanasema mimi msaliti… Leo Mwalimu angetoka akaona haya aliyowatendea, angesema mimi ndiye msaliti ama wao?” alihoji.
Alisema kuwa viongozi wamevuruga muungano aliowaachia, lakini wanapoulizwa   wanamtumia Nyerere kama hirizi bila kutenda wasemacho kama alivyofanya yeye.
“Kwa kuwa wanazo microphone (vipaza sauti) pale bungeni, wanaweza kusema hivyo, lakini je, kweli wanatenda kama Mwalimu au wanasema tu?” alisema.
Kuhusu serikali tatu kuelea kama wanavyodai CCM, kwamba haikopesheki na haina ardhi, Jaji Warioba alisema hoja hiyo ni kuzungumza mambo ya upande mmoja wa Tanganyika, kwa sababu ndani ya serikali mbili Zanzibar itaendelea kutohusishwa katika muungano.
Juu ya madai ya jeshi kupindua serikali endapo mfumo wa serikali tatu utapita, alisema hii ni hatari sana kwa wanasiasa kutumia mbinu za kushawishi umma kwa maslahi ya kisiasa ili waendelee kubaki madarakani.
“Kwa hili ni kama unataka kuchochea kwa kuwa unataka serikali mbili sasa watishe wananchi, msipokubali serikali mbili jeshi litachukua madaraka. Kwa maana nyingine unaliambia jeshi ni baya, litachukua madaraka. Kuna sababu gani ya kufika hapo?
“Unataka kuchochea jeshi liasi kwa kisingizio kwamba hawalipwi mishahara, kwanini jeshi lisilipwe na sio mawaziri au watumishi wengine?” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Bunge la Katiba lilianza kwa kusuasua kidogo kwa kuchukua muda mrefu kutengeneza kanuni na kufarakana kidogo mwanzoni.
“Sisi tulipofanya kazi, tulikwenda kuchukua maoni ya wananchi na wakati ule tulileta mapendekezo ambayo tulidhani ni ya kuwaunganisha wananchi.
“Kwa hiyo tulichotegemea Bunge nalo lingekwenda kwa hatua hiyo, lakini tangu mwanzo likaonekana kwamba limejiunda katika makundi badala ya kujielekeza kwenye suala lenyewe kwa kuangalia mawazo waliyoleta wananchi yanawekwaje ili tupate kitu cha kuwaunganisha,” alisema.
Kuhusu kuchakachua maoni ya wananchi na mabaraza, alisema kuwa katika rasimu ya kwanza walikusanya maoni ya wananchi bila kufuata ni kundi gani wapate maoni.
Alisema kuwa rasimu hiyo ilipotoka wananchi kwa asilimia kubwa waliona maoni yao yamo ila baadhi yalihitaji kurekebishwa.
“Tulipokwenda kwa wananchi hatukuwa na muundo, bali tulitaka watu waseme, ndiyo maana mawazo yote waliyachukua na kuyatafsiri na tulipotoa rasimu ya kwanza tulitaka watu wapitie kila ibara ili waone kama maoni yao yaliwekwa walivyotaka.
“Wananchi wale walikuwa na mambo yao waliyotaka yawemo kwenye katiba, hivyo tuliwapelekea waangalie. Lakini wakubwa hawa wakaenda na kuzunguka wakiwataka washughulikie suala la muungano tu bila kujali kuna mengine. Kwa hiyo waliona hiyo ya madaraka tu wakataka kuifanya hoja ya wananchi,” alisema.
Kuhusu ulazima wa serikali tatu, alisema wakati wa kukabidhi rasimu ya kwanza alisema kuwa ili tuendelee na muundo huu wa sasa wa serikali mbili, kunahitajika ukarabati mkubwa na kwa tathmini ya tume iliona ni vigumu ndiyo maana wakapendekeza serikali tatu.
Alisema kuwa ameona tatizo kubwa kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wakizungumzia takwimu za tume yake wakidai zimechakachuliwa, lakini ukweli ni kwamba zile takwimu ni za kweli.
“Hatukupeleka mapendekezo kwa sababu watu wengi wamesema hivyo, bali tuliangalia hoja. Wanaohoji takwimu hizo wapate majibu kwa Watanzania ambapo Zanzibar wanasema Tanganyika imevaa koti la Mungano na Watanganyika wanasema Zanzibar imemega mamlaka kwa kujigeuza nchi kamili,” alisema.
Mjumbe wa tume
Naye mjumbe wa tume hiyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini kwa madai kuwa wamechoshwa na matusi ya wana-CCM wenzao, alisema kuwa walisimamia sheria na hadidu za rejea, lakini akashangaa kuona wanaandamwa.
Kada huyo wa CCM alieleza kuchoshwa na unafiki wa viongozi wakuu wa serikali zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar akisema kuwa walipokutana na tume yao waliunga mkono serikali tatu, lakini sasa wanajigeuza bungeni na majukwaani wakidai walilishwa maneno.
“Tuna taarifa nyingi kwenye tume na ushahidi wa kutosha, maoni ya Rais wa Zanzibar, Ofisi ya Waziri Mkuu na Baraza la Mawaziri yalikuwa ya serikali tatu ila nimeumia kuona tabia hii mbaya ya kuwa na ndimi mbili,” alisema.
Mjumbe huyo pia alielezwa kushangazwa na kitendo cha Bunge Maalumu kubadili kanuni zake ili kuruhusu kuingiza sura mpya akisema ni kwenda kinyume na rasimu.
“Kuna baadhi ya wabunge wanasikika wakisema kuwa mimi nimetumwa na wananchi wangu kuja kusema msimamo wao ni serikali mbili. Je, walitumwa kwa mujibu wa sheria ipi? Sheria ya Mabadiliko ya katiba inaruhusu wapi mbunge kwenda kukusanya maoni na kuyaleta bungeni?” alihoji.
Alisema ni kama vile viongozi hawajaona kuna tatizo baada ya wajumbe wa UKAWA kutoka nje, kwani CCM wameendelea na majadiliano na kubadili kanuni, huku wakisema wanataka yafanyike maridhiano na wenzao.
“Mwenzako akitoka hakuna tena mjadala. Kama upo kwenye mgogoro wa ndoa, mwenzako ametoka wewe unayebaki unasuluhishwa na nani?” alihoji.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post