Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Joyce Mapunjo
akizungumza na moja ya chombo cha habari wakati wa maadhimisho ya wiki
ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini ambaye ni Msemaji wa Wizara ya
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Vedastina Justinian akimsikilia
mwananchi aliyetembelea banda la wizara hiyo kwenye maadhimisho ya wiki
ya Utumishi ya Umma yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es
Salaam.Picha na Hussein Makame-MAELEZO.
============ =========
Hussein Makame-MAELEZO.
WAKATI
Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki walipotia saini Mkataba wa kuanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1999, kila upande ulilenga maslahi ya
kiuchumi na maendeleo kwa nchi na wananchi wake katika nyanja
mbalimbali. Lakini
ni ukweli ulio wazi kwamba mafanikio ya nchi katika jumuiya hiyo
hutegemea kwa kiasi kikubwa na ushiriki wa wananchi katika hatua za
mtanagamano huo kwani wao ndio walengwa wakuu katika mchakato huo.
Ni
miaka 14 imepita tangu wakuu wa nchi za Afrika Mashariki waliposaini
Mkataba wa kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na miaka 9 tangu kuanza
kwa utekelezaji wa hatua ya kwanza ya mtangamano wa jumuiya hiyo. Pamoja
na mafanikio ambayo Tanzania imeanza kuyapata kutokana na hatua
mbalimbali za mtangamano wa jumuiya hiyo, inaelezwa kuwa bado mwitikio
wa wananchi katika kuchangamkia fursa zilizopo uko chini.
Msemaji
wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Vedastina Justinian
anasema baada ya maandalizi ya miaka sita, nchi tano wanachama wa
jumuiya hiyo zilianza kutekeleza rasmi hatua ya Umoja wa Forodha mwaka
2005.
Katika
hatua hiyo nchi ziliwekeana muda wa kipindi cha miaka mitano za
utekelezaji ambapo nchi ya Kenya ilianza kuingiza bidhaa katika nchi ya
Tanzania na Uganda kwa kutozwa ushuru ambao ulikuwa unapungua mwaka hadi
mwaka. “Sisi
Tanzania na Uganda tulikuwa tunapeleka bidhaa zetu Kenya bure bila ya
kutozwa ushuru kwa sababu Kenya ilikuwa imeendelea kiviwanda, kwa hiyo
ilitupa muda na sisi tuwe tumejiandaa vizuri” anasema Vedastina.
Anafafanua
kuwa mpaka mwaka 2010 Kenya ilianza kuingiza bidhaa katika nchi hizo
mbili bila ya kutozwa ushuru na baadaye nchi wananchama zilianza hatua
ya pili ya mtangamano huo ambayo ni Soko la Pamoja. Soko
la pamoja lilianza kutekelezwa kuanzia Julai mwaka 2010 na lilijumuisha
soko huru la bidhaa, soko huru la mitaji, wananchi kuingia na kukaa
katika nchi anayotaka ilimradi ana pasipoti pamoja na soko huru la
ajira.
Vedastina
anasema kuwa kila nchi ilianisha maeneo ambayo iliyafungua kwa mfano
Tanzania ilifungua maeneo ya walimu wanaofundisha lugha za kigeni,
maafisa ugani, madaktari, marubani na maeneo mengine ambayo yalikuwa
yanaonekana kuwa na upungufu.
Anasema
kwa sasa shirikisho hilo liko kwenye hatua ya Umoja wa Fedha ambao
itifaki yake ilisainiwa Novemba mwaka 2013, muda wa miaka 10 uliwekwa
kufanya maandalizi ya kutekeleza hatua hiyo.
“Maandalizi
hayo ni kuweka uchumi wetu ukae vizuri tuwe na mfumuko wa bei angalau
unayofikia asilimia 8 kila nchi, tuwe na bajeti zisiyotegemea misaada
kwa nakisi za bajeti zetu zisizidi asilimia 3 ya Pato la Taifa”
anafafanua Vedastina na kuongeza kuwa:
“Vile
vile tuwe na akiba za fedha za kigeni ya kutosha ambayo tulijiwekea
kuwa kila nchi iwe na akiba ya fedha za kigeni za kukutosheleza muda wa
miezi minne na nusu, pia nchi tuwe tumejiwekea taasisi muhimu za
utekelezaji wa umoja wa fedha kwa mfano benki kuu kuna taasisi ambazo
zinatakiwa ziwepo.”.
Anasema
baada ya miaka hiyo 10 nchi wanachama zitakaa chini kuangalia kama
zimejiandaa vya kutosha kuanza utekelezaji wa matumuzi ya sarafu
moja na hatua hizo zitakapotekelezwa ipasavyo nchi zitaanza utekelezaji
wa shirikisho la kisiasa.
Akizungumzia
matarajio ya Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Vedastina
anasema baada ya miaka 10 hatua inayofuata ni sarafu moja ambapo gharama
za kufanya biashara zitapungua.
“Sasa
hivi unapokwenda kufanya biashara nje ya Tanzania katika nchi za
Jumuiya kwa mfano Kenya inabidi ubadilishe fedha kwenda shilingi ya
Kenya au Franga za Burundi au Rwanda au uende kwenye fedha ya Uganda”
anasema Vedastina.Anafafanua kuwa kwa sasa mtu anapobadilisha fedha kuna fedha anayokatwa kwa
sababu anayekubadilisha anataka faida, lakini ikifikia hatua ya umoja
wa sarafu kutakuwa na fedha ya aina moja itakayotumia katika nchi zote
za Jumuiya.
Akizungumzia
mwitikio wa Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo, Vedastina anasema
katika eneo la ajira Watanzania bado wanajiweka nyuma kwamba hawataki
kuvuka mipaka kwenda kufanya kazi nchi nyingine.
“Katika
eneo la ajira natoa wito tu kuwa Watanzania wachangamkie hizi fursa
kwani,Watanzania bado wanajiweka nyuma kwamba hawataki kuvuka mipaka
kwenda kufanya kazi sehemu nyingine, ni wachache ambao wameweza
kuthubutu na wameweza kufauru kwenda katika nchi nyingine” anasema
Vedastina.
Anawataka
Watanzania wanapotafuta ajira wasiangalie tu kwa Tanzania na kusema
wamekosa ajira badala yake waangalie soko la Afrika Mashariki kwani
ajira zipo na pia kwa bidhaa kuna soko la watu milioni 140 katika
jumuiya hiyo.
“Wakati
mtu anatafuta ajira aingie kwenye mtandao aangalie hata kwa wenzetu
wanataka watu wa aina gani kama ana sifa zinazohitajika aombe, anaweza
akaajiriwa Kenya, Uganda, Rwanda na hata Burundi” anasisitiza
Vedastina. Anasema
kuwa katika kipindi hiki ambapo wanafunzi wanahitimu katika vyuo vikuu
waanze kuchngamkia soko la ajira la Afrika Mashariki.
Kwa
upande wa wafanyabiashara, Vedastina anasema bado wako nyuma na kutoa
mfano kuwa wakulima wanasubiri wafanyabiashara watoke nchi jirani waende
wakachukue bidhaa mashambani huku wao hawataki kuvuka mipaka.
Anatoa
wito kwamba Watanzania wachangamkie fursa hizo na watoke nje ilimradi
wawe na pasipoti, bidhaa zao zinakidhi ubora na viwango na zina uasilia
wa bidhaa. “Kama
umezalisha bidhaa zako Tanzania tafuta cheti cha uasilia wa bidhaa
ambacho kinapatikana TRA auTCCIA uweze kukidhi vigezo vya kuvuka nje ya
Tanzania na kuweza kuangalia soko kubwa kwani sasa hivi tunategemea
tutaingiza bidhaa hadi Sudan Kusini” anasema Vedastina.
Anasema
Watanzania wana bidhaa nyingi za kilimo na bidhaa zao zina ubora huku
akitolea mfano maonesho ya Juakali Nguvukazi, ambapo watu wanakimbilia
bidhaa za Tanzania ikiwemo asali, batiki, vinyago, mchele na
nyingine. Kutokana
na hali hiyo, Vedastina anawataka Watanzania waache woga wa kwenda nchi
za Afrika Mashariki kwani wafanyabiashara wa nchi nyingine wanachangamkia masoko bila kujali mipaka ya nchi yao.
Anafafanua
kuwa “unajua sasa hivi wafanyabiashara kutoka nje labda Kenya, anakuja
ananunua shamba zima anasema nitavuna mwenyewe, nakulipa tu shamba zima
nitavuna mwenyewe nitapeleka nje.
Kwa
nini ukubali mtu anunue shamba ajivunie mwenyewe, vuna mwenyewe wauzie
wafanyabiashara wavushe mipakani au vuka mwenyewe ukauze nje uvumbuke
macho.
Bila
kuangalia wenzetu wanafanya nini utakaa tu unalaliwa bei unaouza kwa
bei ya chini wenzako wanauza kwa bei ya juu sana, kwa hiyo natoa wito
kwamba Watanzania waaamke wasisubiri watu kutoka nje kingia hadi
mashambani”.
Anasema
iwapo Watanzania watabaki hivyo walivyo matokeo yake hawatapata faida
kubwa ya mazao yao na pia unakosa uzoefu wa kujifunza kwa kuangalia
wafanyabiashara wa nchi nyingine wanafanya nini kuboresha biashara zao.
“Kwa
mfano Tanzania, wafanyabiashara au wakulima hawajajua hata jinsi ya
kufungasha vizuri hizi bidhaa utakuta wenyewe ufungashaji wao ni hafifu
sana, lakini unapotoka nje akaangalia wenzetu wanafanya nini mtu
anajifunza anakuja na yeye anafanya vizuri” anafafanua Vedastina.
Ili
kuhakikisha Watanzania hawaachwi nyuma katika mtangamano wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, Vedastina anawataka Watanzania wajielimishe kuhusu
mambo ya Jumuiya hiyo kwani bado wako nyuma na hawana uelewa wa kutosha.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia