Ticker

6/recent/ticker-posts

Serikali yaweka kipaumbele suala la urasimishaji

 Na Woinde Shizza , Arusha

Serikali imeweka kipaumbele mfumo wa programu za kukuza ujuzi kwa lengo la kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri au kuajiriwa sambamba na kuwajengea uwezo wa kukuza na kuboresha uzalishaji katika fani mbalimbali.



Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako wakati wa hafla ya kutunuku vyeti kwa Wanagenzi wahitimu wa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Njiro, Jijini Arusha .


Prof. Ndalichako alieleza kuwa, Serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia vijana nchini na katika kutekeleza hilo Serikali kupitia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026), ambao unalenga kukuza ujuzi kwa watanzania wapatao 681,000 ambapo kati yao 100,000 ni wa mafunzo ya kurasimisha ujuzi.


Waziri Ndalichako aliwatunuku vyeti wanagenzi wapatao 511 waliofuzu mafunzo na kurasimishwa wakiwakilisha wenzao zaidi ya 2000 .


Aliongeza kuwa, lengo la programu hiyo ya Taifa ya kukuza Ujuzi ni kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki zitakazosaidia kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi kwa kuwezesha nguvukazi nchini kuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa na waajiri mbalimbali nchini.


“Serikali inatambua mchango wa watu waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi na ndiyo maana imechukua hatua hii muhimu ya kuhakikisha wanatambulika rasmi ili nao waweze kushiriki katika shughuli rasmi ikiwemo kufanya kazi katika miradi ya Serikali ya kimkakati,” alieleza


Aidha, Waziri Ndalichako alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana na watanzania kwa ujumla wenye ujuzi katika fani mbalimbali na ambao hawana vyeti vinavyoutambulisha ujuzi wao kuchangamkia programu hiyo kwa kuwa mafunzo hayo hawalipii gharama yoyote isipokuwa muda wao wa kushiriki katika mafunzo.


Waziri Ndalichako alihimiza taasisi mbambali nchini kutumia kikamilifu wahitimu hao kwa kuwa wamebobea katika fani mbalimbali za ufundi.


Awali Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda alisema kuwa kupitia programu hiyo ya taifa ya kukuza ujuzi, Serikali itaweka mifumo bora ya tathimini kwa wahitimu wanaomaliza katika Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopo nchini ili kuwawezesha vijana hao kujiajiri, kuajiriwa na kuajiri wenzao.


Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange alisema kuwa ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha Agizo la Waziri Mkuu alilotoa Agosti 2, 2021 kuwa Halmashauri zote ziwatambue vijana waliofaidika na mafunzo ya programu ya taifa ya kukuza ujuzi na ziwasaidie kuunda vikundi na kuwawezesha kupata mikopo kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani zinazotengwa kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.


Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alisema kuwa Mkoa huo umeendelea kuhamasisha vijana kushiriki kwenye mafunzo hayo ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa.


Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi alisema kuwa katika utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Ofisi hiyo imeendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha wenye Ulemavu wanajumishwa kwa wingi kwenye fani mbalimbali ili waweze kujiendeleza pia.


Naye, Mnufaika wa Mafunzo hayo fani ya Ushonaji Rejina Panga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujali na kutambua mchango wa vijana na kuwapatia ujuzi uliowasaidia kuondokana na changamoto za ajira na kushiriki ipasavyo katika kukuza maendeleo ya taifa.

Post a Comment

0 Comments