Ticker

6/recent/ticker-posts

WAKULIMA,WAFUGAJI WATAKIWA KUFANYA SHUHULI ZAO KWAKUZINGATIA IKOLIJIA NA KUTUNZA MAZINGIRA

 

Mratibu wa mradi wa Islands of peace Erimelinda Temba akielezea umuhimu wa jamii kupatiwa elimu ya ikolojia na bionowai kwa ujumla



Wakulima na wafugaji wametakiwa kufanya shughuli zao kwa  kuzingatia misingi ya kilimo ikolojia na kutunza mazingira yanayowazunguka ikiwemo kuwalinda wadudu wenye faida kama vipepeo na nyuki na hatimaye kuweka kukuza uchumi wao.

Akizungumza katika warsha iliyowajumuisha wadau mbalimbali wa mazingira jijini Arusha,  Mratibu wa mradi  kutoka shirika lisilo la kiserikali la (Island of Peace) linalojishughulisha na uzalishaji wa chakula kwa kutumia mifumo ya kiikolojia, Erimelinda Temba amesema elimu inatakiwa kuongezwa kwa wakulima na wafugaji ili kulinda bionowai kwa ujumla wake.

Bi. Temba amesema katika jukwaa hilo wafugaji, wakulima na wadau mbalimbali wamepata nafasi ya kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na changamoto za  mifumo ya kilimo ikolojia,  faida za wadudu, umuhimu wa mifugo kiikolojoa,  pamoja na jinsi kilimo ikolojia kinaboresha uchumi.

"Wakulima na wafugaji wanategemeana katika shughuli zao kwahiyo kilimo ikolojia kinawapa  faida kubwa na kuinua uchumi wao sambamba na hayo tunawapa elimu juu ya kuwalinda wadudu wenye faida na umhimu wa kilimo bila kutumia viutilifu" amesema Temba.

Licha ya elimu ambayo imeendelea kutolewa na shirika hilo, ameiomba  serikali na wadau mbalimbali wa mazingira kuongeza elimu  kwa jamii ili kufanya kilimo ikolojia kuwa endelevu na kuleta tija kwa upana.

Wadau  walioshiriki walioshiriki warsha hiyo ni wakulima na wafugaji, Maafisa ugani kutoka wizara mbalimbali, Washiriki kutoka vyuo vya elimu ikiwemo chuo cha kilimo  Tengeru na Chuo cha Nelson Mandela.

Katika mjadala uliowagusa zaidi wafugaji kuhusu magonjwa yanayoshambulia mifugo kama mbuzi na Ng'ombe, wameshauriwa kutoa chanjo kwa mifugo yao kila baada ya miezi mitatu ili kuepusha magonjwa yanayoweza kuepukika kama ugonjwa wa ndigana.

Mchangiaji kutoka kabila la wafugaji akieleza changamoto za ufugaji ikolojia

Mwenyekiti wa kikundi cha maendeleo kutoka wilaya ya Longido  Bi.Namboli Nabak amesema elimu waliyoipata katika warsha hiyo itawasaidia katika kilimo wanachofaya na ufugaji ikolojia utawaletea faida zaidi.

" Nimejifunza  ugonjwa wa Ndigana unaotokana na kutochanja  mbwa, ni chanzo cha magonjwa mengi  yanayosumbua sana na kupelekea mifugo yetu kufa naomba wadau warsha kama hizi zirudiwe tena ili elimu iwafikie watu wengi" ameeleza Nabak.

Katika kueleza faida za kilimo ikolojia, Mkulima Antony Mbise kutoka wilaya ya Arumeru, amesema kilimo ikolojia kina faida kwa afya kwani hakitumii mbolea za viwandani wala viuatilifu bali wakulima hutumia samadi, mboji na matandiko badala ya mbolea za viwandani.


" Kwa mfano sisi mazao yetu yakishambuliwa na wadudu tunatumia, ugolo, mkojo wa sungura, majivu tumbaku, ndulele, na pilipili,  badala ya sumu za viwandani ingawa, inatubidi tukae shambani muda mwingi kwa uangalizi ili kugundua kwa wakati pindi mdudu atashambulia mazao, na changamoto ya kilimo hiki, mboga zetu zinakuwa hazina mvuto kama zile zilizotumia madawa ya viwandani" Amesema Mbise.

Post a Comment

0 Comments