Na Novatus Makunga, Ngorongoro
Wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyopo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) wameendelea kuhamasika kuhama kwa hiari kwenda nje ya hifadhi hasa katika kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni Mkoani Tanga
Tayari serikali imewajengea wananchi hao wanaohama kwa hiari miundombinu ya kisasa kama shule, maji, barabara, zahanati, umeme, mawasiliano, huduma za posta, majosho, malisho na mashamba ya kilimo katika kijiji cha Msomera
Wananchi hao ambao pia wamepewa uhuru wa kuchagua wenyewe maeneo mengine wanahama kwa lengo la kupisha shughuli za uhifadhi.
Jumla ya vijiji 25 vipo ndani ya eneo la NCAA vikiwa na wenyeji wa makabila makubwa ya Wamasak ambao kwa asili ni wafugaji, Wadatoga ambao ni wahunzi pamoja na Wahadza e ambao kwa asili ni wawindaji, waokota matunda na wala mizizi
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kapenjiro kata ya Naiyobi wilayani Ngorongoro Mejisho Mollel alisema kuwa hadi sasa katika Kijiji chake zaidi ya kaya 235 zimeshajiandikisha kuhama katika Kijiji hicho.
Naye diwani wa Kata ya Naiyobi tarafa ya Ngorongoro Ngeresa Reteti alieleza kwa sasa serikali imeweka utaratibu mzuri wa wananchi kujiandikisha kwenye ofisi za vijiji.
Kwa upande wake kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Richard Kiiza alibainisha kuwa kwa sasa serikali imeboresha utaratibu kwa kuwafuata sehemu walipo na zoezi la kuwaandikisha linapokamiliaka malipo huandaliwa haraka na ndani ya siku zisizozidi 10.
“Tunahakikisha kuwa mwananchi akiijiandikisha na kuthaminishiwa mali zake, ndani ya siku kumi taratibu zote ikiwepo malipo zinakamilishwa ili mwanachi ahamishe bila kuchelewa," alisema
Kamishina Kiiza alisema wameongeza timu ya wataalamu kutoka Chuo cha maendeleo ya Jamii Tengeru cha Mkoani Arusha ili kuwafikia kwa haraka wananchi wanaotaka kujiandikisha bila kuwachelewesha.