Matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii yamekuwa yakiongezeka kwa asilimia kubwa huku chanzo kikitajwa ni tatizo la afya ya akili.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo Kuu Arusha na Mkurugenzi wa Taasisi ya Ulinzi na Usalama wa Watoto Padre Dennis Ngowi, amesema jamii inatakiwa kuchukua hatua kwa kuwatambua watu wanaonyemelewa na dalili za magonjwa ya akili ikiwemo kusahau mambo na kutamka maneno ya vitisho.
"Tatizo la afya ya akili inayosababishwa na mfumo wa maisha, malezi na makuzi na kutowajibika kwa jamii ipasavyo kuchukua hatua kudhibiti tatizo tangu dalili za awali zinapoanza badala ya kufikiria kwamba ni ushirikina" amesema Padre Ngowi.
Padre ngowi ameeleza kuwa taasisi hiyo imejikita katika kumtetea mtoto kwasababu mtoto hawezi kujisemea tofauti na mtu mzima ambaye anaweza kutoa taarifa pindi anapoona anatendewa kinyume cha matakwa yake.
Aidha ameeleza kwamba taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu kupitia semina za wanafunzi katika shuke za msingi na sekondari, pia vikao vya wazazi vya kila mwezi na siku maalum za wazazi kutembelea watoto mashuleni.
"Elimu imezaa matunda na kuleta matokeo chanya kwa kuibua watu wanatenda au kutendewa mambo kinyume na maadili, lakini bado kazi hii inajitaji watu wengi ili wapokee elimu itakayoenezwa kwa wigo mpana"
Aidha ametoa wito kwa jamii yenye tabia ya kuwaficha watuhumiwa wa ukatili kwa sababu za kuhofia undugu na ujamaa kuvunjika bila kujua kwamba mwisho wa kuficha uovu ni hatari na angamizo kwa baadae.
Kutokana na tabia hiyo ameishauri jamii kupenda kukaa pamoja na kufanya mazunguzo, kusikilizana kufundishana na kuelekezana kwani itasaidia kutambua kama mtu yuko sawa, ama ana shida badala ya watu kuwa bize na simu au vitu vingine vinavyomuacha mtu kukaa peke yake ambapo huko ndiko shida za afya ya akili huanzia kwa kukosa muingiliano wa mawazo kutoka kwa mtu mwingine.
Ameongeza kwamba wazazi wajifunze kulea watoto kwa ukakamavu na kuwajenga kwa maono ili waje kuwa watu wema na wakujega Taifa la baadaye.
"Utamsikia mzazi anasema mtoto wangu hawezi kupitia shida nilizopitia, nitampa kila kitu atakachotaka mara mtoto hazeeki kwa mzazi nitakaa naye, kijana huyo atajitambua na kujua kwamba anatakiwa kubeba majukumu ya familia lini?
"Wazazi kulea imekuwa ni tatizo kubwa, niseme kwa asilimia kubwa wazazi wanachangia vijana wa kike na kiume kuwa mfano mbaya usiyofaa kuigwa katika jamii kwa sababu ya malezi mabaya kutoka kwa wazazi wao" Padre Ngowi amesisitiza.
Hata hivyo Padre Ngowi amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakionyesha kwa taasisi hiyo iliyoko chini ya Parokia ya Mtakatifu Theresa jimbo kuu la Arusha pindi wanapopata taarifa za waliotenda na kutendewa ukatili wa kijinsia.
Taasisi hiyo imebeba kaulimbiu isemayo "Kataa Ukatili Wewe ni shujaa na Jukumu la Ulinzi na Usalama wa Mtoto ni Letu Sote Tanzania Bila Ukatili Inawezekana"
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia