*ARUSHA TUMEKAMILISHA MAANDALIZI YA BUNGE LA 153 LA IPU- RC MAKALLA*
. *_Asema Mkutano huo ni fursa ya kiuchumi kwa wananchi_*
. *_Asema Arusha imejidhatiti kuepusha athari za Elnińo_*
. *_Amshukuru Rais Samia kwa kuimarisha sekta ya Utalii_*
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, amesema maandalizi ya Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), yamefikia hatua nzuri, huku Mkoa ukiendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu fursa zinazotokana na ujio wa mkutano huo.
Amesema elimu hiyo imewafikia wadau wa hoteli, wafanyabiashara wa utalii, wafanyabiashara wadogo pamoja na madereva wa teksi na bodaboda, akieleza kuwa mkutano huo utachochea mzunguko wa fedha kuanzia kwenye hoteli hadi kwa wafanyabiashara sokoni.
Akizungumza leo Ijumaa, Septemba 18, 2026, katika kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC, Makalla amesema Mkoa pia unaendelea kuchukua hatua kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu, ikiwemo kubaini maeneo hatarishi, kusafisha mifereji na kuboresha madaraja na vivuko.
Aidha amesema Mkoa umeanza kampeni ya usafi ili kuhakikisha Arusha inaendelea kuwa kivutio kwa watalii wanaokuja kwa ajili ya utalii wa mbugani, mikutano, tiba, michezo na utalii wa utamaduni, huku akisisitiza kuendelea kuimarisha usalama na ulinzi kama sehemu muhimu ya kuvutia watalii, wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza Mkoani Arusha.
Katika hatua nyingine Mhe. Makalla amesema Arusha inaendelea kunufaika na uwekezaji wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika miundombinu, ikiwemo barabara zinazounganisha maeneo ya vivutio vya utalii ikiwemo ujenzi wa barabara ya tabaka gumu ya kuunganisha hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti huku akiwataka wananchi kuendelea kuwakaribisha wageni kwa huduma nzuri na kutunza sifa ya Arusha kama kitovu cha utalii na uwekezaji.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia