MEYA ARUSHA APONGEZA TIMU YA SHIMISEMITA, ATAKA MAANDALIZI YAENDELEE
Na Woinde Shizza,Arusha
Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Inraqhe, ameipongeza timu ya watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa mafanikio yaliyoyapata katika mashindano ya SHIMISEMITA 2026 yaliyofanyika jijini Mbeya.
Inraqhe amesema ushindi wa makombe matatu, medali na vyeti uliopatikana katika mashindano hayo ni matokeo ya juhudi, nidhamu na kujituma kwa wanamichezo wa timu hiyo.
Amesema licha ya timu hiyo kutokuwa imetwaa makombe yote kama ilivyokusudiwa, mafanikio yaliyopatikana yanastahili pongezi kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo katika mashindano ya mwaka huu.
Meya huyo amesema timu ya Jiji la Arusha imefanya kazi kubwa ya kulitangaza Jiji hilo kupitia ushiriki wake katika mashindano hayo, huku ikichangia pia kushawishi mashindano ya SHIMISEMITA kufanyika Arusha.
Aidha, amewataka viongozi na watumishi wa Jiji kuhakikisha timu hiyo inaendelea kubaki pamoja na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuongeza uwezo na ushindani katika mashindano yajayo.
Inraqhe pia amewapongeza wanamichezo hao kwa kudumisha nidhamu na maadili mema katika kipindi chote cha mashindano, akisema mwenendo huo umeendelea kujenga taswira nzuri ya Jiji la Arusha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, John Kayombo amesema Jiji linaendelea na maandalizi mbalimbali kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Kayombo amesema maandalizi hayo yanahitaji ushirikiano wa viongozi, watumishi na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha Jiji la Arusha linakuwa tayari kupokea na kuhudumia wageni watakaofika wakati wa mashindano hayo.
Amesema watumishi wa Jiji pamoja na wanamichezo wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa kulitangaza Arusha na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya AFCON 2027.
Kayombo amesisitiza kuwa maandalizi ya AFCON 2027 yanaendelea na kila mwananchi anapaswa kutambua nafasi yake katika kuhakikisha Jiji la Arusha linajipanga vizuri kwa ajili ya tukio hilo kubwa la kimataifa.
Meya huyo amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika SHIMISEMITA 2026 yawe chachu ya kuongeza bidii, nidhamu na maandalizi kwa ajili ya kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo.








0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia