ZARA YAIPEPERUSHA BENDERA TANZANIA, YANG’ARA AFRIKA
Na Woinde Shizza,Arusha
Kampuni ya Zara Tanzania Adventures imeendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya utalii barani Afrika baada ya kutwaa tuzo ya Africa’s Leading Adventure Tour Operator 2026, inayotolewa na World Travel Awards.
Ushindi huo umeifanya Zara Tanzania Adventures kutwaa tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kuibuka mshindi pia mwaka 2025, mafanikio yanayoonyesha kuendelea kutambuliwa kwa kampuni hiyo katika sekta ya utalii wa adventure barani Afrika.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, tuzo hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja za timu yake inayojumuisha waongoza watalii wa milimani, wapagazi, waongoza safari, madereva, wafanyakazi wa malodge, ofisini pamoja na watumishi wengine wanaofanya kazi kuhakikisha wageni wanapata huduma bora.
Kampuni hiyo imesema mafanikio hayo pia yanatokana na imani ya wageni na washirika wa safari kutoka mataifa mbalimbali duniani ambao wameendelea kuichagua Tanzania kama sehemu ya kutengeneza kumbukumbu za kipekee za safari.
Zara Tanzania Adventures imekuwa ikihudumia watalii katika maeneo mbalimbali yenye mvuto nchini, kuanzia kilele cha Mlima Kilimanjaro hadi katika tambarare za Serengeti, ambako watalii hupata fursa ya kushuhudia utajiri wa wanyamapori na mazingira ya asili.
Aidha, kampuni hiyo imesisitiza kuwa pamoja na kutoa huduma za utalii, inaendelea kuunga mkono jamii na kutunza mazingira, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa na manufaa ya muda mrefu kwa Tanzania.
Tuzo hiyo imekuja wakati Tanzania ikiendelea kujitangaza kama moja ya vituo muhimu vya utalii barani Afrika, ikiwa na vivutio vya kipekee vinavyowavutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Zara Tanzania Adventures imetoa shukrani kwa timu yake, wageni, washirika wa safari na wadau wote walioendelea kuiamini na kuiunga mkono, ikieleza kuwa ushindi huo ni wa pamoja.
Kwa kutwaa tuzo hiyo mwaka 2025 na 2026, Zara Tanzania Adventures imeweka rekodi ya mafanikio ya miaka miwili mfululizo, huku ikiendelea kujiimarisha katika soko la utalii wa kimataifa na kuitangaza Tanzania kwa kauli mbiu yake ya “Proudly Tanzanian. Proudly African.”



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia