NILE BLUES YAZINDUA MRADI WA FEEL FREE GRANTS, SERIKALI YATOA TAMKO LA KUUNGA MKONO
Na Woinde Shizza, Arusha
MRADI wa Nile Blues Project umezindua rasmi mpango wa Feel Free Grants jijini Arusha, ukiwa na lengo la kutumia muziki, sanaa na utamaduni kuwawezesha vijana kupata maarifa, kukuza vipaji na kujifunza namna ya kutengeneza na kutumia vyombo vya muziki, huku ukibeba kaulimbiu isemayo “Utamaduni Wetu, Urithi Wetu.”
Uzinduzi huo umefanyika katika Shule ya St. Patrick’s, Arusha, ambapo shughuli hiyo ilifunguliwa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na Afisa Utamaduni wa Jiji hilo, Enock Mkumbwa, aliyesema Serikali inatambua na kuunga mkono juhudi za wadau wanaowekeza katika sanaa, utamaduni na maendeleo ya vijana.
Mkumbwa amesema miradi kama Nile Blues Project ina umuhimu mkubwa katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kitamaduni, huku ikiwapa vijana nafasi ya kujifunza kwa vitendo na kutumia vipaji vyao kama sehemu ya kujenga maisha na jamii.
Amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau wa sanaa na utamaduni katika programu zinazolenga kuwajengea vijana uwezo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika utamaduni ni sehemu ya kulinda historia na utambulisho wa jamii.
“Serikali ipo pamoja nanyi na imewaunga mkono tunatambua umuhimu wa mradi huu katika kuwajengea vijana uwezo na kuhakikisha utamaduni wetu unaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine,” amesema Mkumbwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nile Blues Project, Lwanda Magere, amesema mradi huo umejikita katika kuwaunganisha vijana na muziki, sanaa na urithi wa kitamaduni, huku ukiwapa nafasi ya kujifunza ujuzi unaoweza kuwasaidia katika maisha yao.
Magere amesema kaulimbiu ya mradi, “Utamaduni Wetu, Urithi Wetu,” inalenga kuwakumbusha vijana na jamii kwa ujumla kuwa utamaduni ni sehemu ya utambulisho wa jamii na unapaswa kulindwa, kufundishwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.
Amesema kupitia mradi huo, vijana watapata fursa ya kufahamu zaidi muziki wa asili wa Afrika Mashariki, ikiwemo historia na matumizi ya vyombo vya muziki vya asili, pamoja na kujifunza namna ya kutengeneza na kuvitumia.
“Tunataka vijana wajue kwamba utamaduni wetu ni urithi wetu Kupitia muziki na sanaa tunaweza kuwafundisha vijana, kuwapa ujuzi na wakati huo huo kulinda urithi ambao tumerithishwa na vizazi vilivyotangulia,” amesema Magere.
Naye Mkuu wa Shule ya St. Patrick’s, Mathias Sakware, ameushukuru uongozi wa Nile Blues Project kwa kuifikisha programu hiyo shuleni hapo, akisema umefika wakati muafaka na utakuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi.
Sakware amesema wanafunzi watapata nafasi ya kujifunza kwa vitendo, hususan namna ya kutengeneza vyombo vya muziki na namna ya kuvitumia, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kugundua vipaji vyao na kuvikuza mapema.
“Mradi huu umekuja wakati muafaka. Utawasaidia sana wanafunzi wetu kujua namna ya kutengeneza vyombo vya muziki na namna ya kuvitumia Ni fursa kubwa kwao kujifunza kwa vitendo,” amesema Sakware.
Amesema shule iko tayari kuendelea kushirikiana na Nile Blues Project katika utekelezaji wa programu hiyo, akieleza kuwa elimu ya sanaa na muziki inaweza kuongeza ubunifu wa wanafunzi na kuwasaidia kutumia vipaji vyao kwa manufaa ya baadaye.
Kwa upande wake msemaji wa Nile Blues Project Renalda Masawe alisema mpango huo unatarajia kuwafikia wanafunzi katika shule 10 za Arusha, zikiwemo shule tano za msingi na tano za sekondari, kupitia warsha na mafunzo yanayolenga muziki, sanaa, ubunifu na utamaduni.
Mradi huo pia unahusisha elimu kuhusu vyombo vya muziki vya asili kama Adungu na Nyatiti, ukiwa na lengo la kuunganisha vijana na urithi wa muziki wa Afrika Mashariki na kuwapa uelewa wa namna muziki unavyoweza kutumika katika elimu na kujenga jamii.
Feel Free Grants inatekelezwa kupitia Nafasi Art Space, kwa msaada wa Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na Ubalozi wa Norway, Dar es Salaam, huku Nile Blues Project ikilenga kutumia fursa hiyo kuendeleza vipaji vya vijana na kulinda urithi wa kitamaduni.
Uzinduzi huo umeweka msisitizo kwamba sanaa na utamaduni si burudani pekee, bali ni nyenzo muhimu ya elimu, ubunifu, uwezeshaji wa vijana na uhifadhi wa urithi wa jamii.




0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia