KAYOMBO AWAAGA TIMU YA ARUSHA SHIMISEMITA, ATOA WITO WA KUREJEA NA VIKOMBE
KAYOMBO AWAAGA TIMU YA ARUSHA SHIMISEMITA, ATOA WITO WA KUREJEA NA VIKOMBE
Na Woinde Shizza, Arusha
MKURUGENZI wa Jiji la Arusha, Kayombo, amewaaga rasmi wanamichezo wa Jiji hilo wanaoelekea mkoani Mbeya kushiriki Michuano ya Shirikisho la Michezo na Sanaa za Watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA), akiwataka kwenda kupambana na kuhakikisha wanarejea Arusha na vikombe.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanamichezo hao, mkurugenzi wa jiji la Arusha John Kayombo amesema Jiji la Arusha limefanya maandalizi ya kutosha na mwaka huu limeongeza wigo wa ushiriki kwa kupeleka watumishi wengi watakaoshiriki katika michezo yote 15.
Amesema tofauti na miaka ya nyuma ambapo Jiji hilo lilikuwa likipeleka idadi ndogo ya watumishi kushiriki katika michezo michache, mwaka huu limeamua kuongeza nguvu ili kutoa nafasi kwa watumishi wengi kushiriki na kulitangaza Jiji la Arusha kupitia michezo.
Kayombo amewataka wanamichezo hao kutumia vizuri maandalizi waliyofanya, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu, umoja na ushirikiano katika kipindi chote cha mashindano.
Amesema wanamichezo hao wanakwenda Mbeya wakiwa na dhamana ya kuiwakilisha Serikali ya Jiji la Arusha, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanailinda heshima ya jiji hilo kwa kuonyesha nidhamu na ushindani wa hali ya juu.
“Tunawaamini na tunatarajia mtarejea na makombe. Msiende kushiriki tu, nendeni mkashindane na kushinda,” amesema Kayombo.
Kwa upande wake, Afisa Habari na Mstahiki wa Timu ya Watumishi wa Jiji la Arusha, Mwalimu Emmanuel Reziki Joel, maarufu Iman Mzungu, amesema timu hiyo iko tayari kwa mashindano na imejipanga kuhakikisha inapata matokeo chanya.
Amesema wanamichezo hao wana ari, nguvu na hamasa kubwa ya ushindani, huku wakiahidi kupambana katika kila mchezo ili kuhakikisha wanarejea Arusha wakiwa na mafanikio.
Naye Mwalimu na mwanamichezo Djeni Twarira kutoka Serikali ya Kata ya Sinoni, ameishukuru Serikali ya Jiji la Arusha kwa msaada na maandalizi yaliyowezesha idadi kubwa ya watumishi kushiriki mashindano hayo.
Michuano hiyo inatarajiwa kuwa fursa kwa watumishi wa Jiji la Arusha kuimarisha afya, kujenga mshikamano na kuongeza ushirikiano, huku wakibeba dhamana ya kulitangaza Jiji la Arusha katika medani ya kitaifa kupitia michezo.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia