Mahafali ya 15 Arusha Integrated Yahitimisha Wanafunzi 30, Waaswa Kumtanguliza Mungu

 


Na Woinde Shizza, Arusha

Shule ya Arusha Integrated iliyopo jijini Arusha imefanya mahafali yake ya 15 ya wanafunzi wa darasa la saba 30, huku uongozi ukisisitiza suala la kutoa elimu bora na maadili kwa watoto.


Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Rems Munyuku, alisema kwa sasa shule hiyo inamilikiwa na taasisi ya dini ya Arusha Revival Christian Centre, lakini shule yenyewe haina dini na inapokea wanafunzi na kutoa huduma kwa watu wote bila ubaguzi wowote wa dini.


Munyuku alibainisha kuwa wanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo wamekuwa wakifanya vizuri kwa kupata alama A kwenye mitihani yao ya taifa, na anaamini hata wahitimu wa mwaka huu wataendeleza historia hiyo ya mafanikio.


"Tunaamini kila mtoto anastahili kupata elimu bora tunawakaribisha wazazi kuleta watoto wao kwani shule yetu imejipanga kumwandaa mtoto kitaaluma, kimaadili na kivitendo kwa maisha ya baadaye," alisema.


Alisema shule hiyo inapokea watoto kuanzia elimu ya awali wakiwa na umri wa miaka miwili hadi darasa la saba, sambamba na madarasa ya kuhamia kwa wanafunzi kutoka shule nyingine.



Kwa mujibu wa takwimu shuleni hapo, wanafunzi waliohitimu ni 30, kati yao wavulana 12 na wasichana 9 ambao wanauhakika watapata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza, huku shule ikiwa na walimu bora na mahiri.


Akizungumza katika mahafali hayo, mgeni rasmi ambaye ni Kiongozi wa Kanisa la Arusha Revival Christian Centre, Mchungaji David Mollel aliwataka wahitimu hao kuzingatia mambo manne ili waweze kwenda mbali kimaisha na kielimu.


"Mko katika awamu ya kwanza ya safari ya elimu, bado mnasafari ndefu jambo la kwanza la kuzingatia muwe na Mungu katika maisha yenu, kwa sababu ni Mungu ndiye aliyewaumba na maisha ya binadamu yapo mikononi mwa Mungu, ni muhimu kumtanguliza Mungu, ikiwemo swala la ibada msiliweke mbali," alisema Mchungaji Mollel.



Alitaja jambo la pili kuwa ni kuwa na ndoto kubwa na maono makubwa ya kutaka kuwa nani hapo baadaye, kama kuwa daktari au Rais.


"Jambo la tatu, weka bidii maana mwenye bidii atatawala Nne, uwe mtu wa nidhamu, maisha haya hasa safari ya elimu lazima uwe na nidhamu kuna mambo ya kuachana nayo na kuna ya kushikamana nayo, Kila mtoto ahakikishe anakua na nidhamu, asikate tamaa kirahisi na awe na ujasiri, atafanikiwa sana," alisisitiza.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Elimu wa Kanisa la TAG, Beatrice Mollel alisema elimu inayotolewa katika shule hiyo itawasaidia wanafunzi kupambana na changamoto mbalimbali katika jamii.


Alisema wataendelea kujenga taaluma bora na maadili kwa wanafunzi, ikizingatiwa kuwa katika kipindi hiki kumekuwa na mmomonyoko wa maadili kwa watoto.








About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia