MEYA ATOA ONYO KALI WAKATI WA UZINDUZI WA KAMPENI YA “NG’ARISHA JIJI”
Na Woinde Shizza, Arusha
Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe, ametoa onyo kali kwa watendaji wa jiji, maafisa afya, wazabuni wa taka na madiwani kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo usafi wa mazingira jijini humo.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Ng’arisha Jiji” uliofanyika katika Kata ya Sokoni One, eneo la Dampo, Meya Iranghe alisema kampeni hiyo inalenga kuhamasisha wananchi na makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi wa mazingira, ikiwa ni maandalizi ya kulifanya Jiji la Arusha kuwa safi na kuvutia zaidi kuelekea mashindano ya AFCON 2027.
“Watendaji, maafisa afya na madiwani msibweteke ofisini, tokeni nje msimamie usafi Arusha ni jiji la utalii, linapaswa kung’aa muda wote tusisubiri hadi AFCON ifike, tuanze sasa!” alisema Iranghe kwa msisitizo.
Meya alisema utakaohusisha usafi wa jiji kila Jumamosi kwa ushirikiano wa wananchi, taasisi na sekta binafsi ,amesisitiza kuwa usafi ni jukumu la kila siku na si tukio la mara moja.
Aidha, aliagiza magari ya taka kuhakikisha hayamwagi uchafu barabarani, na akaonya kuwa wazabuni watakaokiuka masharti ya mikataba yao watakabiliwa na hatua kali ikiwa ni pamoja na mikataba yao kuvunjwa, Pia alielekeza maafisa afya wa jiji na kata kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu au taasisi zitakazochafua mazingira.
Kwa upande wao, baadhi ya madiwani walipongeza kampeni hiyo na kuahidi kushirikiana kwa karibu na wananchi katika kuhakikisha usafi unakuwa sehemu ya utamaduni wa kila kata.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walipongeza hatua hiyo, wakisema kampeni ya Ng’arisha Jiji itasaidia kuongeza hamasa na kuboresha mazingira ya jiji linalotegemea utalii kama chanzo kikuu cha mapato.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na watendaji wa jiji, madiwani, maafisa afya, wawakilishi wa makundi ya kijamii na wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Jiji la Arusha.
About Woinde Shizza
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.




0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia