Dkt. Kijaji azindua Bodi mpya ya Ngorongoro, awaapisha Kamishna wa Uhifadhi
Dkt. Kijaji azindua Bodi mpya ya Ngorongoro, awaapisha Kamishna wa UhifadhiAagiza ongezeko la vitanda vya malazi na ubunifu zaidi kwenye sekta ya utalii
Na Woinde Shizza, Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameongoza hafla ya kuvishwa cheo Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Abdul Razaq Badru, sambamba na uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa mamlaka hiyo.
Hafla hiyo iliyofanyika Januari 29, 2026, ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha mifumo ya uongozi na usimamizi wa uhifadhi, pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumza katika tukio hilo, Dkt. Kijaji amezielekeza taasisi zote za utalii nchini kuandaa mipango mahsusi ya kutumia matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa kama fursa ya kuongeza mapato na kuvutia watalii wengi zaidi.
Amesema maandalizi ya mapema, ubunifu na matumizi ya teknolojia ni nguzo muhimu katika kuhakikisha sekta ya utalii inazidi kukua kwa tija na ushindani wa kimataifa.
Waziri huyo pia amezitaka taasisi za uhifadhi kuongeza idadi ya vitanda vya malazi kutoka 1,500 vilivyopo sasa hadi zaidi ya 2,000, ili kukidhi ongezeko la watalii na kuongeza muda wanaokaa nchini.
“Tunataka huduma bora, za kisasa na zinazokidhi viwango vya kimataifa ,Hii itachochea mapato na kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uhifadhi endelevu unaohusisha jamii zinazozunguka hifadhi, akibainisha kuwa mafanikio ya sekta hiyo hayawezi kupatikana bila ushiriki wa wananchi na ulinzi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, mkuu wa majeshi mstaafu Venancy Mabeo, amesema sekta ya utalii inahitaji maandalizi ya kudumu, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na usalama kama nguzo kuu za kuvutia watalii.
Wadau wa utalii waliohudhuria hafla hiyo wametoa pongezi kwa uongozi mpya, wakieleza matumaini yao kuwa hatua hiyo itachochea ufanisi katika uhifadhi wa rasilimali za asili na kukuza utalii kwa tija zaidi.





0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia