Waziri Mchengerwa Aagiza Kituo cha Afya Kaloleni Kupandishwa Hadhi



 Woinde Shizza, Arusha.


 Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mchengerwa, ameagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuanza mara moja mchakato wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Jiji la Arusha na maeneo jirani.


Waziri Mchengerwa alitoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa Ongea na Waziri wa Afya uliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, jijini Arusha.


Alisema ongezeko la watu jijini Arusha na mahitaji yanayoongezeka ya huduma za afya yanahitaji vituo vyenye uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ufanisi na kwa wakati.


Aidha, Waziri alimpongeza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kaloleni, Dkt. Anna Kimaro, kwa usimamizi mzuri, uwajibikaji na jitihada zake kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.


Kwa kutambua mchango huo, Waziri alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuandaa Cheti Maalum cha Pongezi kwa Dkt. Kimaro, na pia kuzingatia kumpandisha cheo kuwa Mganga Mfawidhi wa Wilaya kulingana na sifa na vyeti vyake vya kitaaluma.


Hata hivyo, Waziri Mchengerwa alieleza kusikitishwa na taarifa kwamba baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakielekezwa kununua dawa nje ya kituo hicho cha afya, jambo alilolieleza kuwa ni kinyume na taratibu na maadili ya taaluma ya afya.


Alikemea vikali tabia hiyo na kuagiza ikomeshwe mara moja, akisisitiza kuwa ni marufuku kwa mgonjwa wa hospitali ya umma kutumwa kununua dawa nje ya kituo cha afya.


Waziri aliagiza madaktari na wahudumu wote wanaomiliki au kushirikiana na maduka ya dawa jirani na hospitali kufunga biashara hizo mara moja, akionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaokiuka agizo hilo.


Ziara hiyo imeonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, dawa kwa wakati, na kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya afya na haki za wagonjwa.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia