SERIKALI KUJENGA JENGO LA GHOROFA 10 HOSPITALI YA MOUNT MERU — MCHENGERWA




Na  Woinde Shizza, Arusha


Serikali imetangaza mpango wa kujenga jengo la ghorofa kumi katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya afya nchini.


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, alitoa kauli hiyo jana Jijini Arusha alipofanya ziara katika Hospitali ya Mount Meru na Kituo cha Afya Kaloleni, akibainisha kuwa lengo ni kuongeza uwezo wa hospitali hiyo kuhudumia wananchi, wageni na watalii, sambamba na maandalizi ya michuano ya soka ya AFCON 2027.


“Serikali ya Rais Samia imejipanga kuhakikisha kila mkoa una miundombinu ya kisasa ya afya. Hivyo, Mount Meru tunaanza na jengo la ghorofa kumi ambalo litakuwa la mfano nchini,” alisema Mchengerwa.


Aidha, Waziri huyo alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, kuanza mara moja mchakato wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya, akieleza kuridhishwa na huduma na uwekezaji wa vifaa tiba katika kituo hicho.


Katika hatua nyingine, wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa “Ongea na Waziri”, Mchengerwa aliahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya afya kwa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi.


Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Gabriel Makalla, alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, akiahidi kushirikiana na watoa huduma kuhakikisha wananchi wa Arusha wananufaika na miradi hiyo.





“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa kutuletea miradi mikubwa ya afya. Tumeona dhamira yake ya kweli ya kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema Makalla.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia